Waziri Mkuu wa Afrika Kusini ameonya uwezekano wa kutokea majanga zaidi kama mazungumzo ya kumaliza mashambulizi dhidi ya Gaza yatasimama.
Naledi Pandor aliliambia Shirika la Habari la Nchi hiyo(SABC) siku ya Jumanne kuwa walikuwa wamemuomba balozi wao ndani ya Umoja wa Mataifa kufanya jitihada za kuwashirikisha mabolizi wenzake kupitisha azimio la kusitisha mapigano hayo.
“Kwa sasa, kila mtu aazimie kumaliza mashambulizi hayo mara moja,” Pandor alisema.
Aliongeza kuwa dunia itashuhudia majanga zaidi kuliko ya sasa, iwapo mashambulizi hayo hayatasitishwa.
'Hali tete'
“Ningetamani sana kuwatakia raia wa Palestina na Waislamu wote Ramadhani yenye Baraka, lakini kwa watu wa Palestina, naona bado hali ni tete iwapo dunia itaendelea kukaa kimya bila kuchukua maamuzi yoyote kuhusu kumalizwa mara moja kwa mashambulizi haya,” alisema Pandor.
Mwanadiplomasia huyo amesema itakuwa ishara nzuri kwa nchi zenye nguvu kama vile Marekani na Uingereza zitaungana na kuamua kupeleke majeshi yao kuokoa maisha ya biandamu wa Gaza na raia wa Palestina kwa ujumla.
“Kwa wakati huu...bado nina wasiwasi kuwa tunaweza kuendelea kushuhudia madhara zaidi kwa watu wa Palestina...ubinadamu wangu unakosa maana iwapo tunashindwa kuwasaidia watu kutoka kwenye hali mbaya kama ile,” alisema.
Afrika Kusini imelaani mashambulizi ya Israel katika mji wa Gaza na kuishtaki nchi hiyo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ) nchini Uholanzi.
Asilimia 85 wakosa makazi
Maamuzi ya muda mfupi ya Mahakama yaliyotolewa mwezi Januari yameitaka Tel Aviv kuacha vitendo hivyo na kuchukua hatua madhubuti zitakazotoa uhakika wa kutolewa kwa msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia wa Gaza.
Israel ilianzisha mashambulizi dhidi ya ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya kikundi cha Palestina cha Hamas kufanya mashambulizi mpakani mwa Israel. Mashambulizi dhidi ya Gaza hadi sasa yameua takribani watu 30,631 na kujeruhi wengine 72,043 huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa mali na upungufu wa mahitaji muhimu na huduma za kijamii.
Mapigano hayo yamewaacha zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa Gaza bila makazi, huku wakipitia uhaba wa chakula, maji safi na matibabu, wakati asilimia 60 ya miundombinu imeharibika, kulingana na Umoja wa Mataifa.