CODECO inadai kutetea maslahi ya wakulima wa Lendu, ambao kwa muda mrefu wamekuwa katika mgogoro na wafugaji wa Hema./ Picha : Reuters 

Takriban watu 14 waliuawa katika jimbo la Ituri mashariki mwa Kongo siku ya Jumapili, baada ya wanamgambo kuwashambulia waumini waliokuwa wakisali kanisani, afisa wa eneo hilo na kiongozi wa mashirika ya kiraia walisema Jumatatu.

''Kundi la Ushirika wa Maendeleo ya Kongo (CODECO), moja ya wanamgambo wengi wanaoendesha shughuli zao katika eneo la mashariki linalokumbwa na vita, linaaminiwa ndilo lililo husika na shambulio hilo'', alisema msimamizi wa eneo la Djugu Ruphin Mapela na kiongozi wa mashirika ya kiraia Dieudonne Lossa.

"Waathiriwa walikuwa wakimwomba Mungu, lakini kwa bahati mbaya wanamgambo waliotambuliwa kama CODECO waliwafyatulia risasi," Lossa alisema.

Kwa mujibu wa shirika la Reuters, wote walisema kuwa raia 9, wavamizi 4 na mwanajeshi mmoja waliuawa.

Mapela alisema kuwa wanamgambo walishambulia makanisa ya Mesa, Cepac na Aumopro yaliyo karibu na mwambao wa Ziwa Albert katika kata ya Bahema kaskazini.

"Tunatoa wito kwa idadi ya watu kuwa watulivu wakati vikosi vya jeshi vinawafuata wahalifu hawa ili kuwaondoa," msemaji wa jeshi la Ituri Jules Ngongo Tshikudi alisema.

CODECO inadai kutetea maslahi ya wakulima wa Lendu, ambao kwa muda mrefu wamekuwa katika mgogoro na wafugaji wa Hema.

Reuters