Mashambulio ya Israeli dhidi ya Gaza yalisababisha kuhama kwa Wapalestina milioni 1.7. / Picha: AP Archive

Wapalestina siku ya Jumatano wataadhimisha mwaka wa 76 wa kutimuliwa kwao kwa wingi kutoka eneo ambalo sasa linaitwa Israeli, tukio ambalo ni kiini cha mapambano yao ya kitaifa.

Lakini kwa njia nyingi, janga hilo ni dogo kwa ukilinganisha na msiba unaotokea sasa huko Gaza.

Wapalestina wanaiita "Nakba," neno la kiarabu linalomaanisha "janga."

Takriban Wapalestina 700,000, walikimbia au walifukuzwa kutoka makwao kabla na wakati wa vita vya Waarabu na Israeli vya mwaka wa 1948 na kusababisha kuanzishwa kwa nchi ya Israeli.

Wapalestina wengi wahofia kujirudia kwa janga la Nakba au hata zaidi. / Picha: A P

Baada ya vita, Israeli ilikataa kuwaruhusu kurudi.

Badala yake, waligeuka kuwa jamii ya wakimbizi hadi leo, ambayo sasa inafikia takriban milioni 6, huku wengi wao wakiishi katika kambi za wakimbizi na katika makazi duni huko Lebanon, Syria, Jordan na Ukingo wa Magharibi (West Bank) unaotawaliwa na Israeli.

Hivi sasa huko Gaza, wakimbizi na vizazi vyao ina karibia robo tatu ya idadi ya Wapalestina.

Kukataa kwa Israeli kurudi kwa Wapalestina, na Wapalestina kudai haki yao ya mshingi ya kurejea imechangia kuzidi kwa mzozo huo na ni moja ya masuala magumu katika mazungumzo ya amani ambayo yalisambaratika miaka 15 iliyopita.

Wapalestina wamekuwa wakihama kutoka kambi hii hadi nyingine kwa sababy ya uvamizi wa Israeli. / Picha: A P

Sasa, Wapalestina wengi wanaogopa kurudiwa kwa janga hilo baya au hata kwa kiwango cha maafa zaidi.

Wapalestina katika siku za hivi majuzi wamekuwa wakipanda na kupakia magari, mikokoteni ya punda au hata kwenda kwa miguu hadi kwenye kambi za mahema ambazo tayari zimejaa watu, huku Israeli ikipanua mashambulizi yake.

Picha zinazosambaa za uhamishaji wa watu wengi katika vita hivi vya miezi saba ni sawa na picha za nyeusi na nyeupe kutoka mwaka wa1948.

Picha za hivi majuzi zinafanana na zile za mwaka wa 1948. / Picha: A P

Mustafa al Gazzar, ambaye sasa ana umri wa miaka 81, angali anakumbuka safari ya miezi kadhaa ya familia yake kutoka kijiji chao katika eneo ambalo sasa limetawaliwa na Israeli, hapo alikuwa na umri wa miaka 5. Baadhi ya wakati walirushiwa bomu kutoka angani, na wakati mwingine, walichimba mashimo chini ya miti wanapolala ili kupata joto.

Al Gazzar, ambaye sasa ni babu wa mababu, alilazimika kuhama tena mwishoni mwa juma, safari hii hadi kwenye hema huko Muwasi, eneo la pwani ambapo Wapalestina wapatao 450,000 wanaishi katika kambi iliyojaa taka.

Anasema hali ni mbaya zaidi kuliko mwaka 1948, wakati huo shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina lilweza kutoa mara kwa mara chakula na mambo mengine muhimu.

"Tumaini langu mwka wa 1948 lilikuwa ni kurudi, lakini tumaini langu leo ni kuishi," alisema. "Ninaishi kwa hofu," akaongeza, huku akibubujikwa na machozi. "Siwezi kuhudumia watoto wangu na wajukuu."

Vita vya kikatili vya Israeli dhidi ya Gaza vimeua zaidi ya Wapalestina 35,000, kulingana na maafisa wa afya wa eneo hilo, na kuifanya kuwa duru mbaya zaidi ya mapigano katika historia ya mzozo huo.

Vita hivyo vimewalazimu takriban Wapalestina milioni 1.7 - karibu robo tatu ya wakazi wa eneo hilo - kukimbia makazi yao, mara kadhaa. Hiyo ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya waliokimbia kabla na wakati wa vita vya 1948.

Jumuiya ya kimataifa inapinga vikali kufukuzwa kwa wingi kwa Wapalestina kutoka Gaza - wazo lililoshikiliwa na wanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia wa serikali ya Israeli, ambao wanaitaja kama "uhamiaji wa hiari."

Huko Gaza, Israeli imeanzisha oparesheni mbaya za kijeshi na uharibifu zaidi katika historia ya hivi karibuni, wakati mwingine ikishambulia kwa mabomu ya kilo 900 (pauni 2,000) kwenye maeneo yenye makazi.

Vitongoji vyote vimegeuzwa na kuwa jangwa la vifusi na barabara zilizolimwa, nyingi zikiwa na mabomu ambayo hayakulipuka.

Watoto pia wamelazima kuhama kutoka kambi hii hadi ningine kukimbia mashambulizi ya Israeli. / Picha: A A

Benki ya Dunia inakadiria kuwa uharibifu wa dola bilioni 18.5 umefanywa Gaza, takriban sawa na pato la taifa la maeneo yote ya Palestina mnamo 2022.

Na hiyo ilikuwa Januari, katika siku za mwanzo za mashambulizi ya ardhini ya Israeli huko Khan Younis na kabla ya kuingia Rafah.

Yara Asi, profesa msaidizi wa Palestina katika Chuo Kikuu cha Florida ya Kati ambaye amefanya utafiti juu ya uharibifu wa miundombinu ya kiraia katika vita, anasema ni "vigumu sana" kufikiria aina ya juhudi za kimataifa ambazo zingehitajika kujenga upya Gaza.

Hata kabla ya vita, Wapalestina wengi walizungumza juu ya Nakba inayoendelea, ambapo Israeli iliwalazimisha hatua kwa hatua kutoka Gaza, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, maeneo ambayo ilitawala wakati wa vita vya 1967 ambavyo Wapalestina walitaka kuwa ni taifa lao.

Wapaplestina wahofia kutokea kwa Nakba nyingine, ambayo ingesababisha uhamiaji wa idadi kubwa zaidi. / Picha: A A

Ukiangalia ubomoaji wa nyumba, na ujenzi wa makazi kwenye maeneo yaliyotawalwa na sera zingine za kibaguzi ambazo kwa muda mrefu kabla ya vita, na ambazo mashirika makubwa ya haki za binadamu yanasema ni sawa na "ubaguzi wa rangi na kabila".

Asi na wengine wanaogopa kwamba ikiwa Nakba nyingine ya kweli itatokea, itakuwa katika hali ya kuhama kabisa.

"Haitaitwa kuhamishwa kwa nguvu. Itaitwa uhamiaji, au itaitwa kitu kingine," Asi alisema.

"Lakini kimsingi, watu walitaka kubaki, wamefanya kila kitu katika uwezo wao kwa miaka mingi kuishi katika hali ngumu, mwishowe kufikia hali ambayo maisha yamekuwa magumu kwa mtu kustahmili."

TRT World