Uturuki inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zinazohitajika dhidi ya vitendo vya maafisa wa Israeli ambazo zitazidisha hali ya wasiwasi katika eneo hilo./ Picha: AA

Uturuki "imelaani vikali" uvamizi wa Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa Israeli, Itamar Ben-Gvir anayetoka mrengo mkali wa kulia dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu.

"Tunalaani vikali kuvamiwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa na Waziri wa Israel chini ya ulinzi wa vikosi vya usalama," Wizara ya Mambo ya Nje ilisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa.

Wizara hiyo ilisema mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza, pamoja na vitendo vya uchochezi vya mamlaka ya Israeli vinavyonuia kubadilisha hadhi ya kihistoria ya Msikiti wa Al-Aqsa, vinatishia usalama na utulivu wa eneo hilo.

Taarifa hiyo pia imeitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zinazohitajika dhidi ya hatua za maafisa wa Israeli ambazo zitazidisha hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

Ben-Gvir, akiandamana na polisi wa Israeli, walifanya uvamizi katika Msikiti wa Al-Aqsa katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu mapema Alhamisi asubuhi.

Uchokozi unaoendelea wa Ben-Gvir

Ben-Gvir, mkuu wa moja ya vyama viwili vya kidini vya kitaifa katika muungano wa Netanyahu, ana rekodi ndefu ya kutoa kauli za uchochezi zinazokubaliwa na wafuasi wake.

Polisi wa Israeli siku za nyuma waliwazuia mawaziri kupanda hadi kwenye boma la mskiti kwa madai kuwa jambo hilo linahatarisha usalama wa taifa.

Msimamo rasmi wa Israeli unakubali sheria za miongo kadhaa zinazozuia maombi ya wasio Waislamu katika jumba hilo, eneo la tatu takatifu kwa Uislamu na linalojulikana kwa Wayahudi kama Mlima wa Hekalu, ambao wanaamini kuwa ni eneo la mahekalu mawili ya kale.

Nafasi ya Ben-Gvir kama waziri inampa nafasi ya kufuatilia masuala ya jeshi la polisi la taifa la Israeli.

Ben Gvir ambaye pia ni mwanasheria , alijulikana kwa mara ya kwanza kwa kuwatetea vijana wa Kiyahudi wenye itikadi kali wanaoshukiwa kwa uhalifu wa kigaidi na chuki.

Mnamo mwaka wa 2016, aliwawakilisha vijana wawili wenye msimamo mkali walioshtakiwa kwa mauaji ya familia ya Wapalestina katika kijiji cha Ukingo wa Magharibi cha Duma kufuatia shambulio la uchomaji moto.

Kesi hiyo, ambapo mtoto mchanga Ali Dawabsheh mwenye umri wa miezi 18 aliuawa pamoja na wazazi wake baada ya chupa ya Molotov kutupwa ndani ya nyumba zao, ilisababisha mtafaruku wa kimataifa uliosababisha kufunguliwa mashtaka - lakini kwa kweli, kesi nyingi za unyanyasaji wa walowezi dhidi ya Wapalestina ni nadra sana kufunguliwa mashtaka.

Ben Gvir mwenyewe anaishi katika makazi karibu na Hebron katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

TRT World