Serikali mpya ya Uingereza imesema inatupilia mbali ombi la mtangulizi wake kuhusu mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ili kutoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu.
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ameomba vibali vya kukamtwa kwa Netanyahu na waziri wake wa ulinzi, Yoav Gallant, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, kuighadhabisha Israeli na kumuudhi mshirika wake wa karibu, Marekani. Aliomba vibali sawa na hivyo kwa viongozi watatu wa kundi la "muqawama" la Palestina Hamas.
Uingereza, nchi mwanachama wa ICC, ilikuwa imeomba mahakama iruhusiwe kuwasilisha uchunguzi wa kisheria kama ICC inaweza kuwa na mamlaka juu ya Waisraeli "katika hali ambapo Palestina haiwezi kuwa na mamlaka ya uhalifu dhidi ya raia wa Israeli kulingana na Makubaliano ya Oslo".
Lakini tangu wakati huo, chama cha mrengo wa kushoto cha Labour kimechukua mamlaka kutoka kwa chama cha Conservatives katika uchaguzi, na msemaji wa Waziri Mkuu Keir Starmer. aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kuwa serikali mpya itaondoa hoja hiyo "kulingana na msimamo wetu wa muda mrefu kwamba hii ni suala ambalo mahakama itaamua."
"Serikali ina imani kubwa katika utawala wa sheria, kimataifa na ndani ya nchi, na mgawanyo wa madaraka."