Wagonjwa kadhaa walifariki ndani ya siku mbili au tatu zilizopita "kwa sababu ya kufungwa kwa huduma za matibabu", WHO ilisema.
Shirika la Afya duniani WHO, limehimiza uokoaji kamili siku ya Jumapili baada ya kuongoza ujumbe wa kutathmini hali katika hospitali ya Al-Shifa huko Gaza na kulitaja kama "eneo la kifo".
WHO imesema ilifanya ziara fupi yenye "hatari kubwa sana" hadi hospitali hiyo Jumamosi.
Ujumbe huo ulihusisha jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa UN, lililowashirikisha wataalamu wa afya ya umma, maafisa wa vifaa na wafanyakazi wa usalama kutoka mashirika mbalimbali.
Jopo hilo la ukaguzi liliingia hospitali ya Al-Shifa baada ya jeshi la Israeli kuamuru awali kuhamishwa kwa watu 2,500 waliokuwa kwenye majengo ya hospitali, WHO ilisema.
"WHO na washirika wanaendeleza kwa haraka mipango ya uokoaji wa dharura wa wagonjwa waliobaki, wafanyakazi na familia zao," shirika la afya la Umoja wa Mataifa lilisema katika taarifa, na kuongeza kuwa wagonjwa 291 na wafanyakazi wa afya 25 walibakia ndani ya hospitali hiyo.
Kulinga na shirika la afya WHO, jopo hilo lilitaja hospitali hiyo kuwa "eneo la kifo" na hali yake kuwa ya "ya kuvunja moyo.''
"Kuna dalili za makombora na risasi zilionekana wazi. Timu hiyo iliona kaburi la halaiki kwenye mlango wa hospitali na waliambiwa zaidi ya watu 80 walizikwa hapo, " taarifa hiyo ilisema.
Wito wa kutolewa ulinzi wa raia, wagonjwa na wahudumu
Shirika la Afya WHO liliongeza kuwa ukosefu wa maji safi, mafuta, dawa, chakula na misaada mingine muhimu kwa zaidi ya wiki sita imesababisha hospitali kubwa na ya juu zaidi huko Gaza kuacha kuhudumu kama kituo cha matibabu.
Miongoni mwa wagonjwa waliobaki hospitalini ni watoto 32 walioko "katika hali mbaya sana", WHO alisema.
"Tunaendelea kuomba ulinzi wa afya na raia", alisema, akiomboleza kwamba " hali ya sasa haiwezi kuvumilika na haiwezi kuhalalishwa. Mapigano yasitishwe. SASA."Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema Kwenye mtandao wa X.
WHO imefafanua kuwa wahusika zaidi wataingia "ndani ya muda wa saa 24-72 zijazo, ikisubiri dhamana ya njia salama" kusaidia kusafirisha wagonjwa kwenda vituo vingine vya afya kama vile Nasser Medical Complex na Hospitali ya Ulaya ya Gaza kusini mwa Gaza.