Mahakama ya Juu ya Uingereza iliamua Jumatano kwamba mpango wa serikali wa kuwatuma wanao omba hifadhi nchini Rwanda haukuwa halali, na hivyo kuleta pigo kubwa kwa sera ya uhamiaji ya Waziri Mkuu Rishi Sunak na ahadi kuu ya uchaguzi kabla ya kura inayotarajiwa mwaka ujao.
Mahakama kwa kauli moja ilikataa rufaa ya serikali dhidi ya uamuzi wa awali kwamba wahamiaji wasiweze kutumwa Rwanda kwa sababu haiwezi kuchukuliwa kuwa nchi ya tatu salama.
Mpango wa Rwanda ndio nguzo kuu ya sera ya uhamiaji ya Sunak anapojiandaa kukabili uchaguzi mwaka ujao, huku kukiwa na wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wapiga kura kuhusu idadi ya wanao omba hifadhi wanaowasili kwa boti ndogo katika ufuo wa Uingereza.
Mpango tata wa kuwabwaga wahamiaji Rwanda
Mpango wa Rwanda, ulioanzishwa mwezi Aprili 2022 na Waziri Mkuu wa wakati huo Boris Johnson, umeundwa kuwazuia wanaotafuta hifadhi kufanya safari hatari ya takriban maili 20 (kilomita 32) kupitia Mkondo kutoka Ulaya kwa boti ndogo au boti zinazoweza kushika moto hadi fukwe za kusini mwa Uingereza.
Chini ya mpango huo, mtu yeyote ambaye aliwasili Uingereza kinyume cha sheria baada ya Januari mosi 2022, alikabiliwa na kuhamishwa hadi Rwanda, takriban maili 4,000 (kilomita 6,400), ambako madai yao yangetathminiwa.
Hata hivyo, safari ya kwanza ya ndege ya kufukuzwa mnamo Juni 2022 ilizuiwa na amri ya dakika ya mwisho kutoka kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, ikizuia kuondolewa kwa yeyote hadi kukamilika kwa hatua za kisheria nchini Uingereza.
Chini ya sheria mpya iliyopitishwa mnamo Julai, mtu yeyote anayefika kwa boti ndogo madai yake ya hifadhi hayatakubaliwa na atakatazwa kutumia mahakamani sheria za kisasa za utumwa kupinga maamuzi ya serikali ya kuwaondoa nchini.
Mwaka jana pekee, jumla ya watu 45,775 waligunduliwa wakifika fuo za Uingereza bila ruhusa kwa njia hii. Kufikia Novemba mwaka huu, zaidi ya 27,000 wamewasili kwa boti ndogo.
Uhamiaji ni suala nyeti Uingereza
Kurejesha udhibiti wa mipaka ya nchi na kukomesha uhamiaji huru ya watu ilikuwa sababu kuu iliyopelekea kura ya 2016 kwa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.
Serikali za kihafidhina zilizofuata ziliahidi kupunguza uhamiaji wa jumla hadi chini ya 100,000 kila mwaka lakini zilitelekeza ahadi hiyo kabla ya uchaguzi wa 2019.
Ingawa rekodi ya data rasmi imebadilika, uhamiaji wa jumla umeendelea kuongezeka tangu Brexit, na kufikia rekodi ya 606,000 mwaka wa 2022, kutokana na njia mpya za visa kwa waliofika kutoka Ukraine na Hong Kong.
Waingereza wengi, haswa wale walio katika idadi ya watu wanaolengwa na Wahafidhina, kama vile wazee, wanapinga uhamiaji mkubwa, wakisema kuwa unaweka shinikizo kwa huduma za mitaa ambazo tayari zimeenea na kuhofia kuharibu mshikamano wa jamii.
Umuhimu wa mpango wa Rwanda kwa Sunak
Baada ya kuwa waziri mkuu Oktoba mwaka jana altangaza "kusimamisha boti" moja ya vipaumbele vyake vitano kuu.
Kwa sasa Uingereza inatumia zaidi ya pauni bilioni 3 kwa mwaka kushughulikia maombi ya hifadhi, huku gharama ya makazi ya wahamiaji katika hoteli na malazi mengine huku madai yao yakishughulikiwa yakienda kwa takriban pauni milioni 6 kwa siku.
Kuwatuma wanaotafuta hifadhi katika nchi hiyo ya Afrika kungegharimu Uingereza wastani wa pauni 169,000 (dola 213,450), kwa kila mmoja serikali imesema.
Kulingana na takwimu za serikali mwezi Agosti, mrundikano wa maombi ya hifadhi yanayosubiri uamuzi wa awali ulifikia rekodi ya juu ya zaidi ya 134,000, au 175,457 baada ya kujumuisha wategemezi wengine.
Sunak alikuwa ameahidi Disemba iliyopita kufuta hii ifikapo mwisho wa mwaka.