Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak Jumatatu aliahidi kwamba safari za ndege za kuwafurusha waomba hifadhi nchini Rwanda zitaanza baada ya "wiki 10 hadi 12", wakati mpango huo ukiingia katika hatua yake ya mwisho bungeni.
"Tuko tayari, mipango iko tayari na safari hizi za ndege zitaendelea kwa gharama yoyote ile," Sunak aliuambia mkutano wa waandishi wa habari katika eneo la Downing Street, saa chache kabla ya bunge kutayarisha pendekezo hilo tata.
Sunak anasema ni muhimu kupunguza idadi ya wasaka hifadhi wanaoingia Uingereza kutoka Ufaransa kwa boti ndogo.
Alisema kuwa bunge litapitisha kuwa sheria muswada kuhusu usalama wa Rwanda kwa wanaotafuta hifadhi nchini humo siku ya Jumatatu, kufuatia wiki kadhaa za vuta n'kuvute za kutunga sheria kati ya mabunge yake mawili.
Hatari za uchaguzi
"Inatosha. Hakuna kizuizi wala kuchelewa tena," Sunak aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kwamba alitarajia safari za ndege "nyingi" kwa mwezi, katika miezi ya kiangazi.
Uingereza inatazamiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Chama tawala, ambacho kiliiahidi uhamiaji mkali zaidi baada ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, wanatarajiwa kukabiliwa na chama kikuu cha upinzani cha Labour, baada ya miaka 14 madarakani.
Lakini mpango wa kinara wa chama hicho umekumbwa na matatizo na changamoto za kisheria tangu ulipopendekezwa kwa mara ya kwanza na Boris Johnson mnamo Mei 2022 alipokuwa waziri mkuu.
Hadi sasa hakuna wahamiaji waliopelekwa Rwanda.
Zaidi ya watu 120,000 wamevuka kwa kutumia meli toka mwaka 2018, wakati serikali ya Uingereza ilianza kurekodi nambari ya wavukaji, huku kadhaa wakiwa wamepoteza maisha, kulungana na wachunguzi.