Jeshi la Israeli limesema mkuu wa kikosi chake cha kijasusi amejiuzulu kutokana na kushindwa kuzuia shambulio la Hamas la Oktoba 7, ambalo liliweza kupenya ngome za ulinzi za Israeli.
Aharon Haliva, mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa Israeli, amekuwa mtu wa kwanza mkuu wa Israel kujiuzulu siku ya Jumatatu, baada ya shambulio hilo, ambalo Israel inadai kuua watu 1,200, huku takriban 250 zaidi wakichukuliwa mateka.
Haliva alisema muda mfupi baada ya shambulio hilo mwezi Oktoba kwamba alibeba lawama kwa kutolizuia shambulio hilo.
Jeshi la Israel lilisema katika taarifa kwamba mkuu wa majeshi alikubali ombi la Haliva la kujiuzulu na kumshukuru kwa utumishi wake.
Kujiuzulu kwake kunaweza kuweka mazingira kwa wakuu zaidi wa usalama wa Israel kukubali lawama kwa kutozuia shambulio hilo na kuachia ngazi.