Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Mahamat Moussa Faki ameunga mkono matamshi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina / Picha: AFP

Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Mahamat Moussa Faki, anasema ameunga mkono "uongozi" wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wakati ambapo Gutteres ameshutumiwa kwa matamshi yake kuhusu hatua za kijeshi za Israel huko Gaza kwenye Baraza la Usalama la UN.

Guterres alilaani mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Hamas alipohutubia Baraza la Usalama siku ya Jumanne, lakini alisema "hayakutokea bila sababu."

"Ninaunga mkono kikamilifu msimamo na uongozi wa Antonio Guterres na kazi ya Umoja wa Mataifa katika maeneo yanayokaliwa ya Palestina," Moussa Faki Mahamat aliandika kwenye X siku ya Alhamisi.

"Unaendana na sheria za Kimataifa na msimamo wa Umoja wa Afrika na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa," aliongeza.

Miaka 56 ya 'kutopumua'

Gutteres katika hotuba yake alipaza sauti kwa ajili ya maafa ya Palestina na kusema, "Wananchi wa Palestina wamekabiliwa na miaka 56 ya kukaliwa kimabavu."

"Wameona ardhi yao ikiendelea kuchukuliwa na makazi kuathiriwa na ghasia, uchumi wao kudorora, watu wao kuhama na makaazi yao kubomolewa. Matumaini yao ya suluhu la kisiasa kwa masaibu yao yamekuwa yakididimia," aliongeza.

Maoni hayo yaliibua hasira kutoka Israel, huku ikimtaka Guterres ajiuzulu.

Guterres baadaye alisema, "ameshtushwa na tafsiri potofu" ya matamshi yake na akarudia ombi lake la kusitishwa kwa mapigano mara moja kwa kibinadamu ili "kupunguza mateso, kufanya utoaji wa misaada kuwa rahisi na salama, na kuwezesha kuachiliwa kwa mateka."

Takriban watu 8,000 wameuawa

Mzozo wa Gaza ulianza wakati kundi la wapiganaji wa Palestina, Hamas, lilipoanzisha 'Operesheni Al-Aqsa Flood,' shambulio la kushtukiza la pande nyingi lililojumuisha kujipenyeza ndani ya Israeli kupitia ardhini, baharini na angani.

Hamas imesema uvamizi huo ulikuwa wa kulipiza kisasi kuvamiwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa na kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo ya Gaza.

Mpaka sasa, takriban watu 8,000 wameuawa katika mzozo huo, wakiwemo takriban Wapalestina 7,028 na Waisrael 1,400.

TRT Afrika