Familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa katika eneo lililozingirwa la Gaza wametishia mgomo wa kula hadi serikali ya mrengo wa kulia ya Israel itakapofanya makubaliano mapya ya kubadilishana na kundi la muqawama wa Palestina, Hamas, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Gazeti la Yedioth Ahronoth lilisema siku ya Ijumaa tishio hilo lilitolewa baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukataa kukutana na familia hizo.
Ilisema familia 100 zilimshutumu Netanyahu kwa kutaka kuligawanya kundi hilo ili asilazimike kujibu madai yao.
Yedioth Ahronoth alisema familia hizo zilimpa Netanyahu hadi Jumamosi jioni kufanya mkutano nao na kufanyia kazi kuachiliwa kwa mateka.
Familia hizo zilisema uvamizi wa kijeshi wa Israel huko Gaza unakinzana na juhudi za kuwaachilia mateka hao, kwa mujibu wa gazeti hilo.
Serikali ya Israel yenye misimamo mikali bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tishio la mgomo wa njaa unaofanywa na familia hizo.
Maandamano baada ya mateka kuuawa na wanajeshi
Wakati huo huo, wanafamilia wa mateka pia walikusanyika karibu na Wizara ya Ulinzi huko Tel Aviv baada ya tangazo la kuuawa kwa mateka watatu na jeshi la Israeli.
Msemaji wa jeshi Daniel Hagari alitangaza kuwa wanajeshi wa Israel "kwa kimakosa" waliwaua mateka watatu wa Israel wakati wa vita huko Gaza.
Hagari aliielezea kama "ya kusikitisha" na akasema jeshi "lina jukumu."
Wakati wa mapumziko ya wiki moja ya kibinadamu katika Gaza iliyozingirwa mwezi uliopita, Hamas iliwaachilia Waisraeli 81, raia 23 wa Thailand na raia wa Philipino, kubadilishana na Wapalestina 240, wakiwemo wanawake 71 na watoto 169, wanaoteseka katika jela za Israel.
Takriban Wapalestina 18,800 wameuawa tangu wakati huo na 51,000 kujeruhiwa katika shambulio la Israeli, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza.
Idadi ya vifo vya Israeli katika milipuko ya Hamas imefikia 1,200, ambayo ilirekebishwa kutoka 1,400.
Zaidi ya mateka 130 bado wanashikiliwa na kundi la Wapalestina huko Gaza, kulingana na takwimu rasmi.