Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amekutana na wenzake kutoka Kazakhstan, Iraq, Lebanon, Gambia, na Tajikistan kabla ya mkutano wa Kidiplomasia wa Antalya unaoanza Machi 1 mpaka 3.
Fidan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan Murat Nurtleu walijadiliana uhusiano wa nchi hizo mbili na mikakati ya kukuza usharikiano kwenye sekta ya ulinzi, siku ya Alhamisi.
Vyanzo vya kidiplomasia vinaripoti kuwa kuwa mawaziri hao waliangazia maeneo mengine na hatua za kuchukua kukuza ushirikiano katika elimu na utamaduni.
Suala la kukua kwa biashara kati ya nchi hizo mbili na kuvuka kiwango cha dola bilioni 10 mwaka jana, kilijadiliwa wakati wa mkutano huo.
Mawaziri hao pia walitathmini miradi inayokuja katika biashara, nishati na sekta ya usafiri.
Vilevile, Fidan na Nurtleu walijadiliana masuala ya kikanda na uwezekano wa kushirikiana ndani ya baraza la mfumo wa Kituruki.
Majadiliano kuhusu ziara ijayo ya Rais Erdogan nchini Iraq
Wakati wa mkutano na mwenzake wa Iraq Fuad Hussein, maandalizi ya ziara iliyopangwa ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan nchini Iraq yalijadiliwa.
Baada ya mkutano wa amani kati ya Uturuki na Iraq uliofanyika mjini Ankara mwezi Disemba, Fidan na Hussein pia walijadili ratiba ya mkutano mwingine wa usalama unaotarajiwa kufanyika mjini Baghdad hivi karibuni.
Mkutano pia uligusia hali ya usalama ya Iraq, na maendeleo ya hivi karibuni katika kanda na maendeleo ya Mradi wa Barabara.
Yanayoendelea Gaza
Fidan alikutana na mwenzake kutoka Lebanon, Abdallah Bouhabib na walijadiliana mahusiano ya nchi hizo mbili na yanayojiri Gaza.
Katika mkutano huo, mawaziri hao walijadili athari ya yanayotokea Gaza na hatma ya usalama katika ukanda huo.
Mkutano na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Gambia na Tajikistan
Fidan pia alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Gambia Mamadou Tangara na wa Tajikistan Sirojiddin Muhriddin.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uturuki ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili katika maeneo yote, huku Gambia ikiwa ni moja ya washirika muhimu wa Uturuki barani Afrika.
Mataifa hayo pia yalikubaliana kuongeza ushirikiano wa kijeshi, uchumi na kitamaduni.
Katika mkutano na Muhriddin, ziara za ngazi ya juu kwa mwaka huu zilijadiliwa na hatua za kuchukua kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kiusalama, elimu na uchumi.
Baada ya Muhriddin kutoa taarifa kuhusu hali ya sasa ya mazungumzo ya kuweka mipaka kati ya Tajikistan na Kyrgyzstan, Fidan alieleza kuridhishwa kwa Ankara na maendeleo katika suala hili na kueleza kwamba makubaliano yaliyofikiwa yangechangia utulivu na ustawi wa eneo hilo.
Mawaziri hao pia walijadiliana yanayojiri Afghanistan na athari zake kwa Tajikistan.
Wawakilishi kutoka nchi 147
Mkutano wa Kidiplomasia wa Antalya utakuwa mwenyeji wa nchi 147.
Takriban washiriki 4,500, wakiwemo wakuu 19 wa nchi, mawaziri 73 na wawakilishi 57 wa kimataifa, wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo.
Kongamanno hilo, lenye dhima ya Kukuza Diplomasia wakati wa Matatizo, unalenha kuangazia masuala mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabia nchi, uhamaji, Chuki dhidi ya Uislamu, vita vya kibiashara na akili mnemba.
Kongamano la mwaka 2021, lilikuwa na washiriki 2,000. Mwaka 2022, majopo 30 ya midahalo iliandaliwa, wakati kwa mwaka huu yatakuwa 52.
Kongamano hilo litajumuisha washiriki mbalimbali wakiwemo wanadiplomasia na wanasiasa, wanafunzi, wasomi na wawakilishi kutoka mashirika ya kiraia na jumuiya ya wafanyabiashara.
Maonesho mbalimbali yatafanyika katika mkutano huo.