Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amehudhuria mkutano wa kimataifa wa maendeleo na uhamiaji mjini Rome, ambao uliandaliwa na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni.
Fidan siku ya Jumapili, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda wakati wa mkutano wa faragha ili kukabiliana na uhamiaji usio wa kawaida, ambao alielezea kama changamoto inayokabiliwa na nchi za Mediterania, kulingana na duru za kidiplomasia.
Ili kusitisha mtiririko wa wahamiaji katika vyanzo , waziri wa mambo ya nje wa Uturuki alisema migogoro na matatizo ya kiuchumi lazima yaondolewe ili kufanikisha hili.
Fidan pia alisisitiza umuhimu wa kugawana mzigo wa wahamiaji wasio wa kawaida, akitoa wito kwa mataifa yote kuzuia chuki dhidi ya wageni na uhalifu wa chuki na kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana kwa ajili ya kulinda utu wa binadamu.
Mkutano huo, ambao ni "mpango wa sera ya kigeni" wa Italia, uliwakaribisha viongozi na wanadiplomasia wakuu kutoka nchi za Mediterania, Mashariki ya Kati na Ghuba.
"Mkutano huo, ambao utawaleta pamoja wadau wakuu kuhusu uhamiaji na maendeleo, unalenga kutoa suluhu endelevu katika kupambana na uhamiaji usio wa kawaida na hivyo kuamua hatua zinazoweza kuchukuliwa kuzuia uhamiaji katika chanzo," Wizara ya Mambo ya Nje ya Türkiye ilisema katika taarifa yake Jumamosi.