Mkutano wa 15 wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ulianza Jumamosi katika mji mkuu wa Gambia, Banjul.
Viongozi wa dunia kutoka nchi 57 wanachama wa OIC na kwingineko wanatarajiwa kuhudhuria, ilisema OIC katika taarifa yake kabla ya mkutano huo. Anayemwakilisha Türkiye katika hafla hiyo ni Hakan Fidan, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo.
Iliongeza kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha umoja "katika kushughulikia kwa pamoja changamoto kubwa zinazoukabili Ummah (jumuiya ya Kiislamu) na kupanua ushirikiano na mshikamano kati ya nchi wanachama katika kutekeleza malengo yetu ya pamoja kama yalivyoainishwa katika katiba.
Umoja na mshikamano
OIC iliongeza kuwa mkutano huo pia unalenga "kupanua uchumi wetu wa ndani na kufufua biashara ndogo na za kati," pamoja na "kuchukua fursa ya kugawana utajiri wa utamaduni wa Gambia na Afrika na ulimwengu."
Mkutano huo unaoendelea hadi Jumapili ukiwa na mada kuu "Kuimarisha umoja na mshikamano kwa njia ya mazungumzo kwa ajili ya maendeleo endelevu," utashughulikia masuala ya kimataifa, hasa hali ya sasa ya Palestina na vita vinavyoendelea vya Israel huko Gaza, ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 34,000.
Wakati wa mkutano huo, nyaraka tatu muhimu - rasimu ya azimio la Palestina, rasimu ya taarifa ya Banjul, na rasimu ya waraka wa mwisho - zitawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje na baadaye kwenye mkutano wa kilele kwa ajili ya majadiliano.