Muhammed Azo alitekeleza shambulio la kombora kwenye Kituo cha Polisi cha Yakacik cha Kamandi ya Kikosi cha 1 cha Mpakani kwenye barabara ya Sirnak/Cizre-Silopi mnamo Februari 2022, na kuua mwanajeshi mmoja wa Uturuki na kuwajeruhi wengine watatu. / Picha: TRT World

Shirika la Kitaifa la Ujasusi la Uturuki (MIT) "limemkata makali" gaidi wa ngazi ya juu wa PKK katika operesheni zake kaskazini mwa Syria, vyanzo vya usalama vilisema katika taarifa Jumamosi.

Aliyetambuliwa kama Muhammed Azo, anayejulikana pia kwa jina lake la siri Sibli Derik, alilengwa na MIT mwaka jana, lakini alitumwa nje ya nchi na shirika la kigaidi la PKK/YPG kwa matibabu ya majeraha yake.

Baada ya kupona alirudi Derik Kaskazini mwa Syria

"Mwishowe, mhusika wa hatua iliyolenga vikosi vyetu vya usalama vinavyohudumu katika mipaka yetu, Mkuu wa Kikosi cha PKK/YPG Derik Brigade Sibli Derik, Muhammed Azo, alikatwa makali katika operesheni hiyo," ilisema taarifa hiyo.

Muhammed Azo alikuwa anatafutwa kwa shambulizi dhidi ya kituo cha polisi kwenye barabara ya Cizre-Silopi katika jimbo la Sirnak mwaka jana mwezi Februari na kuua mwanajeshi mmoja na kuwajeruhi wengine watatu.

Muhammed Azo alikuwa akihudumu kama afisa wa brigedi katika shirika hilo la kigaidi.

Pia alikuwa afisa wa uratibu wa zoezi la pamoja ambapo magaidi 250 wa PYD/YPG walishiriki, kwa msaada wa Marekani, huko Derik Kaskazini mwa Syria mnamo Septemba 7, 2022, kulingana na taarifa.

Tangu 2016, Ankara imezindua oparesheni tatu zenye mafanikio za kupambana na ugaidi katika mpaka wake Kaskazini mwa Syria ili kuzuia uundaji wa ukanda wa ugaidi na kuwezesha makazi ya amani ya wakaazi: Euphrates Shield (2016), Olive Branch(2018) na Peace. Spring (2019).

Mamlaka ya Uturuki yanatumia neno "kuwakata makali" kumaanisha magaidi wanaohusika walijisalimisha au waliuawa au kukamatwa.

Katika kampeni yake ya zaidi ya miaka 35 ya ugaidi dhidi ya Uturuki, PKK - iliyoorodheshwa kama shirika la kigaidi na Uturuki, Marekani na EU - imehusika na vifo vya zaidi ya watu 40,000, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto.

YPG ni chipukizi la PKK la Syria.

TRT World