Watu mbalimbali walikuwa katika hali ya ukimya, kama ishara ya kuwakumbuka waathirika wa tukio hilo, lililotokea mwaka 2023/Picha: AA

Uturuki imeadhimisha miaka miwili tangu kutokea kwa mkasa mbaya wa matetemeko ya ardhi ambayo yalitikisa kusini mwa nchi hiyo, siku ya Februari 6, 2023 kwa kuwakumbuka wale waliathirika na janga hilo, ambapo watu wapatao 53,537 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 107,000 kujeruhiwa.

Wakazi katika miji iliyotikiswa na matetemeko hayo, walikusanyika katika medani za miji saa kumi na dakika kumi na saba alfajiri ya Alhamisi, muda ambao tetemeko la kwanza lilitikisa, kwa kukaa kimya kwa muda, kuwakumbuka waliopoteza maisha yao.

Wengine, walitembea kimya kimya katika miji tofauti, kuwakumbuka walioathirika na mkasa huo.

katika wilaya ya Pazarcik, kwenye jimbo la Kahramanmaras, ambapo ndio kitovu cha tetemeko, wakazi wa eneo hilo walikusanyika mbele ya mnara wa saa, ambao ulisimama, huku Uturuki ikikumbuka miaka miwili tangu kutokea kwa mkasa huo.

Huko Hatay, moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi, wawakilishi kutoka dini zote tatu za Kiislamu, Kiyahudi na Kikristo walifanya maombi kama sehemu ya kumbukumbu ya siku hiyo.

Kisha wakarusha mawaridi mekundu kwenye Mto Orontes, unaojulikana kama Asi River nchini Uturuki, kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao.

Tarehe 6 Februari, 2023, matetemeko yenye vipimo vya 7.7 na 7.6 yalitikisa majimbo 11 ya Uturuki – Adana, Adiyaman, Diyarbakir, Elazig, Hatay, Gaziantep, Kahramanmaras, Kilis, Malatya, Osmaniye na Sanliurfa.

Watu zaidi ya milioni 14 waliathirika nchini Uturuki kutokana na matetemeko pamoja na wengine wengi kaskazini mwa Syria.

Uturuki kuendelea na ujenzi wa maeneo yaliyopatwa na matetemeko

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametuma ujumbe kwenye mtandao wa X Alhamisi kuwakumbuka watu 53,537 waliofariki kwenye matetemeko ya ardhi, na kuwaombea rehema roho zao.

"Kuanzia siku ya kwanza, tumeungana kama taifa na kama watu wa taifa hili, sisi ni ' watu wamoja,' na katu hatutawahi kuacha kuwasaidia watu katika maeneo yaliyoathirika na matetemeko," alisema.

Aliahidi kuendelea kusaidia juhudi za ujenzi, akisema wataendelea "kwa ari yote, kufanya kazi kwa bidii, na uthabiti" hadi mpaka pale kila raia atapata nyumba iliyo salama kuishi.

Baadaye siku ya Alhamisi, Erdogan atahudhuria hafla ya kumbukumbu katika mji wa Adiyaman.

AA