Tukio la uzinduzi litafanyika katika Kituo cha Teknolojia cha TOBB ETU, ambapo kompyuta ya quantum itaonyeshwa. / Picha: AA

Uturuki inajiandaa kuzindua kompyuta yake ya kwanza ya quantum Alhamisi, hatua kubwa kuelekea kuboresha uwezo wa taifa katika usalama wa data, akili mnemba (AI), ulinzi, na zaidi.

Kompyuta hiyo ya quantum, iliyoendelezwa na Chuo Kikuu cha TOBB cha Uchumi na Teknolojia (ETU) kilichoko katika mji mkuu wa Ankara, imeundwa na miundombinu inayosaidia maendeleo yake endelevu. Hii inaashiria hatua kubwa kuelekea uhuru wa kiteknolojia wa nchi hiyo. Pia inasaidia maono ya Uturuki kuwa kiongozi katika mfumo wa teknolojia ya quantum.

Hafla ya uzinduzi itafanyika katika Kituo cha Teknolojia cha TOBB ETU, ambapo kompyuta hiyo ya ''quantum'' itaonyeshwa.

Mpango huu unatarajiwa kuzalisha nafasi mpya za ajira na kuimarisha ujasiriamali.

TOBB ETU inalenga kujenga mfumo wa quantum unaoweza kushindana kimataifa, kusaidia biashara changa kuunda vifaa vya quantum vya ndani na vijenzi vyake.

Tofauti na kompyuta za jadi, ambazo hutumia biti za kawaida kuhifadhi na kuchunguza data, kompyuta za quantum hutumia biti za quantum, au qubits, hivyo kuruhusu utendaji wa kazi ngumu zaidi.

Kompyuta ya kwanza ya quantum ya Uturuki inatarajiwa kuboresha nafasi ya nchi hiyo katika sekta hii inayoibuka.

Kompyuta za quantum zina matumizi mengi katika nyanja mbalimbali, zikiwemo: usimbaji fiche (cryptography) kwa ajili ya kulinda data kwa usalama zaidi, akili mnemba (AI) kwa uchakataji wa hali ya juu wa algorithimu, ulinzi kwa kuendeleza teknolojia za kimkakati, utafiti wa hali ya hewa kwa kuchanganua mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili, pamoja na kugundua vifaa vya kizazi kijacho.

TRT World