Uturuki inatarajiwa kuufungulia mtandao wa kijamii wa Instagram baada ya jukwaa hilo kukubali kufuata matakwa ya nchi hiyo, haswa kuhusu sera zake kuhusu uhalifu.
"Kufuatia mazungumzo yetu na maafisa wa Instagram, tutaiiondoa Instagram kifungoni saa 9:30, kulingana na ahadi yao ya kutimiza matakwa yetu," waziri wa uchukuzi na miundombinu wa Uturuki, Abdulkadir Uraloglu, alisema katika taarifa kwenye mtandao wa X siku ya Jumamosi.
Uturuki iliifungia Instagram kutokana na sera za mtandao kuhusu uhalifu, hususani baada ya kuondoa maudhui yanayohusiana na kiongozi wa chama cha Hamas Ismail Haniyeh katika siku ya kitaifa ya maombolezo.
Mamlaka za Uturuki na META, kampuni mama ya Instagram, walishiriki katika majadiliano ili kuweka masharti yatakayopelekea kufunguliwa tena kwa jukwaa hilo.
'Udhibiti, safi na rahisi'
"Tokea mwanzo, tuliiomba mitandao ya kijamii kuheshimu sheria za Jamhuri ya Uturuki," aliandika Uraloglu kwenye mtandao wa X.
Kwa mujibu wa Uraloglu, Uturuki na META wamefikia makubaliano kuhusu mfumo wa uhalifu na kuahidi kushirikiana katika udhibiti.
Mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki Fahrettin Altun aliukosoa vikali mtandao wa Instagram, akishutumu jukwaa hilo kwa "kuzuia kikamilifu watu kutuma ujumbe za rambirambi kwa kuondokewa na kiongozi wa Hamas [Ismail] Haniyeh bila kutaja ukiukaji wowote wa sera."
"Huu ni udhibiti, safi na rahisi," Altun alisema katika chapisho kwenye X kufuatia mauaji ya Haniyeh huko Tehran.