Kufuatia kuchaguliwa tena kwa Recep Tayyip Erdogan kama rais wa Uturuki mwezi uliopita, sasa macho yameelekezwa kwa uhusiano wa Ankara na shirika la kujihami la NATO, hususan kuhusiana na ombi la Uswidi kujiunga na shirika hilo.
Jumbe za pongezi zimeendelea kumiminika kutoka kwa viongozi wa dunia, waliotaka kuendeleza ushirikiano na Uturuki.
Hata hivyo ushindi wa Erdogan umeleta uwezekano wa kubadili mwelekeo wa baadhi ya nchi, kuashiria umuhimu wa kufanyia marekebisho sera zao za uhusiano na Uturuki.
Erdogan amefanya mazungumzo na viongozi kadhaa baada ya hafla ya kuapishwa iliyohudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu kutoka mataifa takribani themanini pamoja na waakilishi wa mashirika makubwa ya kimataifa, akiwemo katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg.
Akitaja Uturuki kama mshirika mkuu wa kuthaminiwa, Stoltenberg alipongeza mchango wa Ankara katika kutafutia suluhisho mzozo wa Urusi na Ukrain, hasa katika kufanikisha mpango wa nafaka wa bahari nyeusi, ulioruhusu mamilioni ya tani za nafaka kutoka Ukrain kusafirishwa kwa nchi zinazohitaji.
Pia alizungumzia matarajio yake kwa Uturuki juu ya ombi la Uswidi kutaka kujiunga na NATO akiongeza kuwa anatumai kuhitimisha utaratibu wa nchi hiyo kupokewa katika NATO haraka iwezekanavyo.
Katika wiki hiyo hiyo, Recep Tayyip Erdogan na rais wa Marekani Joe Biden walijadili uuzaji wa ndege ya kivita aina ya F-16 na uwezekano wa Uswidi kujiunga na NATO, wakati Biden alipompigia simu kumpongeza rais huyo wa Uturuki kwa ushindi wake katika uchaguzi.
Wataalamu wanasema kuwa sasa macho yataelekezwa kwa namna gani Uturuki itaendeleza uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi kadhaa.
Kuidhinishwa kwa Uswidi.
Kwa miaka mingi rais Erdogan amekuwa thabiti katika msimamo wake kuwa mataifa yote wanachama wa NATO lazima yatilie maanani hofu za kiusalama za Uturuki. Na wengi katika NATO waliamini kuwa matokeo tofauti katika uchaguzi wa Uturuki, yangesababisha mustakabali tofauti kabisa wa Uswidi kujiunga na NATO.
“NATO walinuia kuwa, iwapo upinzani ungeshinda uchaguzi huo, wangeikaribisha Uswidi bila wasiwasi kama mwanachama. Lakini kwa kuwa Erdogan ndiye rais, lazima washughulikie wasiwasi wake," Profesa Sami Al Arian, mkurugenzi wa taasisi ya uislamu na masuala ya kimataifa (CIGA) katika chuo cha Zaim mjini Istanbul ameambia TRT World.
Kwasababu ya muda mchache uliosalia kabla ya kikao maalum cha NATO, Uswidi haina budi kufanyia marekebisho sera zake.
“Kama tulivyoona katika siku chache zilizopita, Uswidi imepiga hatua muhimu kwa kupitisha sheria inayoharamisha usaidizi wowote kwa makundi ya kigaidi kama vile PKK,” balozi wa zamani wa Marekani Matthew Bryza ameambia TRT World.
Hata hivyo, “Suala muhimu lililobakia ni masharti ya Uturuki kuwa, washukiwa wa PKK na FETO warejeshwe nchini Uturuki kutoka Sweden,” aliongeza.
Jumanne, mahakama ya juu nchini Uswidi ilitoa ruhusa kwa serikali kuwarejesha wanachama wa PKK nchini Uturuki. Uamuzi huo wa mahakama sasa umetwika jukumu kwa serikali ya Uswidi kuamua iwapo iwarudishe washukiwa hao au la. Iwapo itatekelezwa, itakuwa tukio la kwanza la Uswidi kuwarejesha washukiwa wa PKK nchini Uturuki.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanao watetea wanachama wa makundi ya kigaidi ya PKK/YPG, wamekuwa wakifanya maandamano kupinga sharia hiyo dhidi ya ugaidi.
Mwezi uliopita, watu wanaounga mkono PKK walifanya kampeni ya propaganda wakimlenga rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mafiasa wa Uswidi katika majengo ya bunge mjini Stockholm.
Uturuki imeiomba serikali ya Uswidi isiwakubalie wanachama wa PKK kufanya propaganda za kigaidi chini ya ulinzi wa polisi.
Lakini kuna dalili kuwa huenda makosa ya Uswidi ni zaidi ya kuliruhusu kundi la kigaidi la PKK ndani ya mipaka yake. Mwaka jana, Maafisa wa usalama wa Uturuki walinasa makombora ya kutingua vifaru vya kivita, yaliyotengenezwa na Uswidi, katika mapango yanayoaminiwa kuwa maficho ya wanamgambo wa PKK, kaskazini mwa Iraq.
Katika hotuba kwa wanahabari wiki hii, waziri mkuu wa Uswidi Ulf Kristersson alidai kuwa nchi yake imetekeleza ‘masharti yote iliyoafikiana na Uturuki’, na kuwa ''uamuzi uko kwa Uturuki, iwapo Uswidi itakubaliwa au la. Sio sisi kuamua.’’ Aliongeza.
Lakini kwa serikali ya Ankara, maneno hayo hayana uzito wowote, hasa ukizingatia visa vya hivi majuzi vya uchokozi vilivyofanywa na wanachama wa PKK nchiin Uswidi.
Uhusiano na Marekani
Uzito wa Uturuki kama mshirika huru wa NATO unaendelea kujitokeza bila kutegemea uhusiano wake na Marekani. Huku mazungumzo juu ya masuala kadhaa yakiendelea kati ya nchi hizo mbili, miradi mipya inaweza kuanzishwa na viongozi hao.
"Uturuki imeamua kufuata mkondo wake kuthibiti nguvu zake na ushawishi katika eneo hilo," anasema Prof Al Arian, akiongeza kuwa hii ni ‘‘mojawapo ya sababu ya kurejelea uhusiano kati ya Marekani na Uturuki baada ya uchaguzi.”.
"Kuongoza kwa Erdogan kwa miaka mingine mitano, kuna maana kuwa Marekani italazimika kutimiza masharti ya kiusalama ya Uturuki," aliongeza Al Arian.
Mapema wiki hii, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken na waziri mpya wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan, walijadiliana masuala kadhaa ikiwemo ombi la Uswidi kujiunga na NATO, mpango wa kusawazisha mahusiano kati ya Uturuki na Armenia na Uturuki na Azerbaijan, ununuzi wa ndege za kivita za F-16 na makubaliano ya nafaka ya Ukrain.
Katika mazungumzo hayo kwa njia ya simu , Blinken alidai kuwa serikali ya Marekani, haijaunganisha uuzaji wa ndege hizo za F-16 na ombi la uwanachama wa Uswidi katika NATO.
Uturuki na utawala wa Marekani unafuatiliwa kwa makini majukumu yao juu ya mustakabali wa NATO.
"Nadhani tutaona Uhusiano ulioimarika kati ya Marekani na Uturuki, na hatua ya kwanza ya rais Biden itakuwa kuidhinishwa kuuziwa Uturuki ndege za kivita za F-16 ," Bryza amesema.
Pande zote mbili zimekuwa zikibadili sura kuhusiana na wasiwasi wa kiusalama, mahitaji ya ulinzi na sera zao juu ya Mashariki ya Kati, hasa kaskazini mwa Syria.
Licha ya upinzani mkali wa Uturuki juu ya kuwepo kundi la YPG, linaloaminiwa kuwa sehemu ya kundi la kigaidi la PKK ndani ya Syria, Marekani imeungana na kundi hilo, kupigana na Daesh.
Na kama ilivyo ada ya Marekani kujaribu kubainisha tofauti kati ya ‘magaidi wazuri ‘ na ‘magaidi wabaya’, Marekani imetoa mafunzo mengi ya kivita na usaidizi wa silaha kwa YPG, wakidai ni muhimu kati kavita dhidi ya Daesh.
Licha ya wasiwasi wa halali wa kiusalama wa Uturuki kama mshirika wa NATO, Marekani imeendelea kuiunga mkono YOG/PKK, iliyo orodheshwa kama kundi la kigaidi na Uturuki, Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, na kulaumiwa kwa vifo vya zaidi ya watu 40,000 wakiwemo wanawake na watoto.
Umuhimu wa upatanishi wa Uturuki
Bila kujali siasa zao za kimaeneo, mojawapo ya mambo muhimu ya NATO, pamoja na ya mataifa yasiyokuwa wanachama, juu ya Uturuki, ni kutambua umuhimu wake katika kuwezesha makubaliano ya nafaka na Ukrain, yanayo shikilia umuhimu mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chajula duniani.
Kupitia uongozi mwingine chini ya Erdogan,kuna uwezekano mkubwa kuwa Uturuki itathibitisha udhamini wake wa nafaka hiyo.
"Hatua ya Uturuki, kufanikisha makubaliano ya njia ya nafaka, ni kitu ambacho mataifa yote, sio ya Magharibi pekee, yanatambua. Wangependa kuona Uturuki ikiendelea na jukumu hilo," Bryza anasema.
"Tunahitaji nafaka hiyo ya Ukrain ifikie masoko ya kimataifa, ili kuisaidia Ukrain pamoja na kuhakikisha kuna usalama wa chakula duniani, ili kuepusha majanga ya njaa, hasa katika mataifa yanayostawi.."