Fidan amethibitisha tena utayari wa Uturuki kuchangia amani na ujenzi mpya nchini Ukraine kwa njia yoyote ile. / Picha: TRT World

Katika mahojiano ya kipekee na TRT World, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesisitiza kwamba changamoto zilizopo za Ulaya - kutoka kwa vita vya Ukraine hadi mizozo katika Mashariki ya Kati, pamoja na uwezekano wa kujitenga kwa Marekani kisiasa - zimeilazimu nchi za Ulaya kufahamu tena umuhimu mkubwa wa Uturuki.

"Marafiki zetu wa Ulaya wanagundua tena umuhimu wa Uturuki," Fidan aliiambia TRT World wakati wa mahojiano ya moja kwa moja pembezoni mwa Mkutano wa Usalama wa Munich siku ya Jumapili.

Fidan ameeleza kuwa tangu aingie madarakani, Trump amekuwa akihoji mfumo wwa kimataifa, akisema kuwa Marekani inatoa zaidi ya inavyoingiza. Msimamo huu umeleta mshtuko duniani kote na kusababisha mpasuko Ulaya.

Huku mataifa ya Ulaya yakizidi kufahamu udhaifu wao wa kimkakati ikiwa ni pamoja na migogoro inayoendelea, kama vile vita vya Ukraine na ukosefu wa utulivu katika Mashariki ya Kati, wanatumai mpasuko huo ni wa muda lakini wanabaki kuwa waangalifu wanapopitia mabadiliko yanayojiri, Fidan alisema.

"Huu ni wito wa ulimwengu mzima kuzinduka," , akisisitiza ya kwamba mazingira ya kijiografia na kisiasa yanayoendelea yanahitaji mataifa kufikiria upya ushirikiano wa jadi na kukabiliana na mienendo mipya ya mamlaka.

"Wanaona kwamba Uturuki ni mshirika anayetegemewa na mwenye nguvu," Fidan aliongeza. Amebainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan, Uturuki imekabiliana na changamoto zake za miundombinu na kuimarisha msingi wake wa ulinzi na biashara ya viwanda - yote bila kupokea mamia ya mabilioni ya fedha kutoka Umoja wa Ulaya.

Vita vya Ukraine

Suala kuu katika Mkutano wa Usalama wa Munich lilikuwa vita vya Ukraine. Akibainisha kuwa pande zote mbili sasa zinasisitiza haja ya kusitisha mapigano, Fidan alisema hatua kubwa imepigwa.

"Ninawajua baadhi ya wahusika wa ambao hawakutaka kusikia neno la kusitisha mapigano," aliiambia TRT World. Fidan alithibitisha tena utayari wa Uturuki kuchangia amani na ujenzi mpya nchini Ukraine kwa njia yoyote ile.

"Lakini kwanza kabisa, tunahitaji kuwa na usitishaji mapigano. Na tunahitaji kuwa na mpango unaotekelezeka na wa muda mrefu wa amani,” alisisitiza.

Akibainisha kuwa Marekani na Ulaya sasa zimeungana kufanya kazi kuelekea mpango wa amani, Fidan alisema hata hivyo ni kazi ngumu ambayo "ina changamoto kubwa".

Akizungumzia nafasi ndogo ya Ulaya katika mchakato wa amani, Fidan alisema kuwa nchi za Ulaya zinastahili nafasi katika meza ya mazungumzo, huku pia akisisitiza kuwa Uturuki vile vile imekuwa na nafasi sahihi katika mazungumzo hayo - na kwamba Uturuki inaweza kuchangia zaidi kuliko wahusika wengine wengi.

"Haya yanafanyika katika nchi jirani… Na tuna uhusiano wa karibu kwa pande zote mbili," Fidan alibaini.

Kuhusu makubaliano yanayoweza kutokea kuhusu uhuru wa eneo la Ukraine, Fidan alikubali uwezekano wa kuwa na "maamuzi magumu."

"Katika ulimwengu wa kawaida, tungependa kuona kwamba uhuru wa eneo (la Ukraine) unalindwa. Lakini huu ni wakati wa vita,” alisema, akiongeza kuwa muda pekee ndio utakaofichua iwapo upatanishi wa Marekani utatosha kuleta Urusi na Ukraine kwenye maelewano.

Syria, kupambana na ugaidi

Katika mahojiano yake ya moja kwa moja , Fidan ameangazia zaidi wasiwasi wa Uturuki kuhusu uwepo mkubwa wa kundi la kigaidi la PKK nchini Syria, ambapo utawala mpya pia unatanguliza vita dhidi ya makundi yenye silaha.

"Nadhani si watu wengi wanaojua ukweli kwamba PKK inamiliki theluthi moja ya ardhi yote ya Syria na kukaa kwenye rasilimali muhimu za nishati ambazo zinahitajika sana na watu wa maeneo mengine ya Syria," alisisitiza.

Akielezea PKK kama tishio lililopo sio tu kwa Uturuki lakini pia kwa Wakurdi huko Syria, Iraqi na Iran, Fidan alisema: "Katika nchi yoyote, hatuwezi kuwa na vikundi vyenye silaha ambavyo haviripoti kwa serikali kuu."

Pia amesisitiza umuhimu wa kupambana na ugaidi kikanda, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuzuka upya kwa Daesh, akionya kwamba uingiliaji kati wa kigeni mara nyingi husababisha matatizo zaidi.

"Sasa, ni wakati wa kukomesha vitendo vya kigaidi vya Daesh na PKK," Fidan alisema, akihimiza juhudi za pamoja "kumaliza virusi hivi."

Vita dhidi ya Gaza

Akizungumzia mzozo wa kibinadamu katika Gaza huko Palestina, Fidan alisema kwamba hatimaye kulikuwa na "taswira ya matumaini ya siku zijazo" na usitishaji wa mapigano unaendelea. Hata hivyo, alionyesha mashaka juu ya uendelevu wake.

"Viashiria vyote, kwa bahati mbaya, vinapendekeza kwamba (Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin) Netanyahu hana nia ya kuendelea na usitishaji mapigano," alisema, akionya kwamba Israeli inaweza kuanzisha tena vita mara tu mateka wote watakapoachiliwa huru.

Fidan alitoa wito kwa utawala wa Trump kuwajibika na kuishinikiza Israeli kutoendeleza upanuzi zaidi, akisema "inatakiwa kuwa jukumu la Bwana Trump na utawala wake kuzuia mauaji mengine ya halaiki, na uhalifu mwingine dhidi ya ubinadamu."

Vinginevyo, ahadi ya uchaguzi wa Trump juu ya kusimamisha vita katika nchi za kigeni na watu kupoteza maisha "itakuwa ya mashaka," aliongeza.

TRT Afrika