Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan (katikati) mwezi uliopita, alikuwa mwenyeji wa Waziri wa Mambo ya Nje wa EthiopiaTaye Atske Selassie (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moalim Fiqi (Kulia) jijini Ankara. / Picha" AA

Ujumbe wa maofisa wa Somalia umesafiri kutoka Mogadishu kuelekea Uturuki kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo kati ya Somalia na Ethiopia.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za kutatua mzozo kati ya majirani hao wawili wa Afrika Mashariki kuhusu mkataba wa bandari, ambao Addis Ababa imetia saini na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland, kitendo kilichoikasirisha Mogadishu.

‘’Ujumbe huo ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ahmed Moallim Fiqi Ahmed, siku ya Jumamosi, ulielekea mji mkuu wa Uturuki, Ankara,’’ ilithibitisha Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia katika taarifa yake.

Ratiba rasmi

‘’Ujumbe unaowakilisha Serikali ya Somalia, umepokea mwaliko rasmi kutoka kwa Serikali ya Uturuki, na utashiriki katika duru ya pili ya mazungumzo na Ethiopia, ambayo yanaandaliwa na Serikali ya Uturuki,’’ iliongeza taarifa hiyo.

Majadiliano hayo yanatarajiwa kuanza mjini Ankara siku ya Jumatatu, wiki tatu kabla ya ratiba ya awali.

Hali kadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan siku ya Ijumaa, alitangaza kuanza kwa mazungumzo hayo.

Tangazo hilo limetolewa wiki moja baada ya Waziri huyo kuitembelea Addis Ababa na kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Ufikiaji bahari

Uturuki ilianza rasmi juhudi za upatanishi za kutatua tofauti za Ethiopia na Somalia mwezi uliopita kwa duru ya kwanza ya mazungumzo mjini Ankara, ambapo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan alikuwa mwenyeji wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili.

Mvutano kati ya Somalia na Ethiopia ulitokana na mpango wa kufikia bandari ambao Addis Ababa ilitiana saini na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland, mwezi Januari.

Mpango huo, ungeipa Ethiopia nchi isiyokuwa na bahari, haki ya kuingia baharini kupitia Somaliland, na kwa upande wake, ingeitambua Somaliland kama nchi huru, hatua ambayo ilipingwa vikali na Somalia.

TRT Afrika