Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan, amesisitiza kwamba serikali ya mpito ya Syria haina mpango wa kuwa na utawala wa majimbo yanayojitegema, akigusia msimamo wa Uturuki katika kudumisha uhuru wa kujitawala wa Syria.
Katika mahojiano yake na Shirika la Habari la Anadolu, siku ya Jumatano jijini Ankara, Fidan aliangazia majadiliano muhimu kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa serikali ya mpito ya Syria Ahmed Al Sharaa, akisisitizia umuhimu wa kushirikiana katika ujenzi mpya wa nchi hiyo, ulinzi wa mipaka na mapambano dhidi ya magaidi wa PKK/YPG na Daesh.
Matarajio kutoka Syria
Fidan aligusia matarajio ya Uturuki kutoka utawala mpya wa Syria, akiangazia umuhimu wa Syria kuwajibikia changamoto zake ili kuhakikisha kuwa hakuna vitisho dhidi ya Uturuki na usalama wa kanda.
"Matarajio yetu makubwa kutoka kwa Ahmad Al Sharaa ni kuwa tayari kutatua matatizo ya nchi yake. Tunategemea kuona wakitatua matatizo yao ambayo yanatishia usalama wa Uturuki pamoja na kanda nzima," alisema.
Aliongeza kuwa Uturuki ina matarajio hayo hayo kutoka kwa majirani zake, wakiwemo Iraq na Iran, na kusema kuwa Uturuki haiko tayari kutishia majirani zake na wala haitegemei kufanyiwa hivyo.
Alisisitiza haja ya Syria kusambaratisha magaidi wa PKK pamoja na washirika wao ndani ya mipaka yake ili kulinda umoja na mamlaka yake.
Fidan pia alisema kuwa magaidi wa PKK/YPG walitumia fursa ya machafuko wakati wa utawala ulioangushwa wa Assad kutekeleza mashambulizi yao katika eneo la Kaskazini mwa Syria.
Pia alipongeza msimamo wa Al Sharaa dhidi ya magaidi wa PKK/YPG, akisema kuwa unarandana hofu ya usalama ya Uturuki. Alibainisha kuwa Syria imejitolea kuwaondoa na kuwakata makali magaidi wa kigeni wa PKK ili kudumisha umoja wa kitaifa.
Aitaka Marekani kuacha kuisadia YPG
Katika hatua nyingine, Fidan alizungumzia nafasi ya Marekani nchini Syria, akiitaka Marekani kufikiria upya uwepo wa majeshi yake na kusitisha kutoa msaada kwa YPG, ambalo ni sehemu ya chipukizi ya shirika la kigaidi la PKK.
"Syria mpya inatakiwa kusonga mbele bila kuchelewa. Tunategema Marekani waache kuisaidia YPG na kuondoa vitisho kwa Syria," alisema Fidan, na kuongeza kuwa Uturuki imeimarisha mazungumzo na maafisa wa Marekani kuhusu suala hilo.
Ushirikiano wa kikanda dhidi ya ugaidi
Fidan alitangaza mpango mpya wa kikanda unaohusisha Uturuki, Iraq, Syria na Jordan kupambana na Daesh. Nchi hizo nne zinapanga kuweka utaratibu wa pamoja wa juhudi za kukabiliana na ugaidi, kuratibu hatua kupitia masuala ya kigeni, ulinzi na njia za kijasusi.
Kuhusu ushirikiano wa usalama kati ya Uturuki na Iraq, Fidan alisisitiza kuwa Iraq lazima ichukue hatua madhubuti kukomesha shughuli za PKK ndani ya mipaka yake. Alikariri kuwa kupambana na ugaidi bado ni kipaumbele cha kwanza kwa Uturuki na kwamba utulivu wa kikanda unategemea kuondoa vitisho vya ugaidi.
Fidan alihitimisha kwa kusisitiza kwamba majaribio yoyote ya kuigawanya Syria kwa misingi ya kikabila au kisiasa hayatakuwa na tija, akionya kwamba kugeuza makabila kuwa zana za kisiasa kwa ukosefu wa utulivu hakuna faida yoyote. Alisisitiza kujitolea kwa Uturuki kwa ujenzi mpya wa Syria na utulivu wa muda mrefu, akionyesha nia ya Uturuki kusaidia mchakato wa ujenzi wa nchi hiyo.
Mkutano kati ya uongozi wa Uturuki na Syria unaashiria hatua muhimu katika kuweka sawa mienendo ya kikanda na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.