Erdogan amesisitiza haja na umuhimu wa umoja wa taifa la Kiislamu kuzuia mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na kuiadhibu kutokana na mashambulizi hayo. / Picha: AA   

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani wamejadiliana uhusiano wa nchi hizo mbili na hali ya kibinadamu huko Gaza.

Katika mazungumzo yao ya simu siku ya Jumatatu, viongozi hao walizungumzia uhusiano kati Uturuki na Qatar, masuala ya kimataifa, kikanda, mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na hali ya kibinadamu katika eneo la Palestina, kulingana na taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.

Kwa upande wake, Erdogan alisisitiza haja ya umoja katika ulimwengu wa Kiislamu kuongeza juhudi za kukomesha mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na kuadhibu uhalifu dhidi ya ubinadamu ambao imefanya katika muda wote wa mashambulizi yanayoendelea.

Rais wa Uturuki ameongeza kuwa ni muhimu kuizuia Israel haraka iwezekanavyo na kuchukua hatua kwa busara ili kuzuia mvutano kuenea katika eneo hilo.

Wawili hao, pia walitumia fursa hiyo kupongezana kufuatia sherehe ya Kiislamu ya Eid al Fitr, iliyoadhimishwa wiki iliyopita.

Mashambulio hatari ya kijeshi

Israel imefanya mashambulizi mabaya ya kijeshi huko Gaza tangu shambulio la Oktoba 7 likiongozwa na Hamas ambapo takriban Waisrael 1,200 waliuawa.

Takriban Wapalestina 33,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa huko Gaza, na karibu 76,500 kujeruhiwa huku kukiwa na uharibifu mkubwa na uhaba wa mahitaji.

Vita vya Israel vimesababisha asilimia 85 ya wakazi wa Gaza kuhama makazi yao huku kukiwa na shida kubwa katika usambazaji wa chakula, maji safi na dawa, huku asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo ikiwa imeharibiwa , kulingana na Umoja wa Mataifa.

TRT Afrika