Kumekuwa na visa vingi vya hapo awali vya vikosi vya Israel kujaribu kuwazuia wafanyakazi wa TRT kuripoti kuhusu Gaza na Jerusalem Mashariki  iliyokaliwa kwa mabavu/ Picha: AA

Polisi wa Israel wamejaribu kuwazuia waandishi wa habari wa Uturuki kuripoti matukio katika jiji la kale la Jerusalem Mashariki linalokaliwa kwa mabavu, huku afisa mmoja wa polisi akivunja kamera ya waandishi hao.

Waandishi hao wa habari kutoka Shirika la Utangazaji la Taifa la TRT News walikuwa wakiripoti kuhusu vikosi vya Israel kuwazuia na kutumia nguvu dhidi ya Wapalestina waliokuwa wakielekea msikiti wa Al Aqsa kwa ajili ya swala ya Ijumaa.

Polisi wa Israeli waliwashambulia jopo la waandishi wa TRT News, wakivunja kamera yao kwa kutumia bunduki walipokuwa wakifanya kazi ya kuripoti matukio katika eneo hilo lenye hali tete.

Ingawa kamera iliharibiwa, mwandishi wa TRT alisema wataendelea kutoa taarifa kuhusu mashambulizi yanayoendelea Palestina. Wakati wa matangazo ya moja kwa moja, polisi wa Israel walirusha mabomu ya machozi katika eneo la msikiti.

Mwandishi wa TRT alibainisha jinsi Israel inavyopiga marufuku mikusanyiko ya swala nje ya Msikiti wa Al Aqsa, akilalamikia vikwazo vilivyoenea vinavyowakabili waumini wa Kiislamu wanaofanya ibada kwa amani.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Altun alaani shambulio hilo

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun amelaani shambulizi lililotekelezwa na polisi wa Israel kuwalenga waandishi wa habari wa TRT.

"Israeli inaendelea kukiuka sheria za kimataifa na washirika wake wote wenye silaha, kutoka kwa jeshi lake hadi polisi, inaonekana kudharau sheria na kanuni," Altun aliandika kwenye X.

"Hakika, shambulio hili baya limeongezwa kwenye rekodi ya aibu ya Israeli kuhusu uhuru wa vyombo vya habari."

Altun alikariri wito wa nchi yake kwa jumuiya ya kimataifa kuzungumza zaidi dhidi ya Israel, ambayo inaendeleza mauaji yake bila ya ubaguzi, inayolenga watoto wachanga, wanawake, wazee na walemavu, na kuzuia kazi ya waandishi wa habari.

Pia aliwatakia heri familia ya TRT.

Kumekuwa na visa vingi vya hapo awali vya vikosi vya Israeli kujaribu kuwazuia wafanyakazi wa TRT kuripoti Gaza na kukalia kwa mabavu Jerusalem Mashariki.

Wiki hii, vikosi vya Israeli kwa mara nyingine vilisimama katika njia ya swala ya Ijumaa, vikiwawekea vizuizi Wapalestina wanaotaka kwenda katika Msikiti wa Al Aqsa katika Mji Mkongwe wa Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu.

Maombi ya amani yanafanyika wakati mashambulizi ya hivi karibuni ya Israeli huko Gaza, na ukandamizaji mkali katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, una zaidi ya siku 40.

Takriban Wapalestina 195 wameuawa na wengine zaidi ya 2,500 kujeruhiwa na moto wa jeshi la Israel katika ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Jerusalem Mashariki iliyokaliwa kwa mabavu, tangu Oktoba 7, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina.

Israel imeanzisha mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya Gaza tangu shambulio la kuvuka mpaka la kundi la Hamas la Palestina Oktoba 7.

Takriban Wapalestina 11,500 wameuawa, wakiwemo wanawake na watoto wapatao 7,900, na wengine zaidi ya 29,800 wamejeruhiwa, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka kwa mamlaka ya Palestina.

TRT Afrika