Shirikisho la Soka la Uturuki limesitisha mechi zote za ligi hadi ilani nyingine kufuatia shambulio dhidi ya mwamuzi aliyeidhinishwa na FIFA.
"Klabu inayowajibika na wasimamizi wake wataadhibiwa vikali zaidi. Kila mtu ambaye amewahi kuwalenga waamuzi anahusika katika uhalifu huu wa kuchukiza," rais wa shirikisho hilo, Mehmet Buyukeksi, alisema baada ya mkutano usio wa kawaida wa bodi ya watendaji wake.
Rais wa klabu ya daraja la juu ya Uturuki MKE Ankaragucu, Faruk Koca, alimshambulia kimwili mwamuzi Halil Umut Meler baada ya timu yake kutoka sare dhidi ya Caykur Rizespor siku ya Jumatatu.
Kufuatia kumalizika mechi hiyo, Koca aliingia uwanjani na kumpiga ngumi ya uso Meler.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya alisema kwenye X kwamba Koca alikuwa akipokea matibabu katika hospitali chini ya uangalizi wa polisi baada ya kujisikia kuzirai kufuatia kitendo chake cha vurugu uwanjani, na kuongeza kuwa "taratibu za kumweka kizuizini zitatekelezwa baada ya matibabu."
Yerlikay pia alisema kuwa watu wengine wawili waliompiga Meler teke la kichwa wakati wa tukio hilo walizuiliwa kwa maagizo ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ankara Magharibi.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani kisa hicho kilichotokea katika mji mkuu wa Ankara.
"Michezo ina maana ya amani na udugu. Michezo haiendani na vurugu," Erdogan alichapisha kwenye Twitter, ambayo inaitwa 'X'.
"Kamwe hatutaruhusu vurugu kutokea katika michezo ya Uturuki," aliongeza.
Shambulio la nadra
Mwamuzi wa FIFA tangu 2017, Meler mwenye umri wa miaka 37 ndiye aliyesimamia mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa wa Lazio dhidi ya Celtic mnamo Novemba 28.
Waamuzi wa Uturuki mara nyingi hukosolewa na wasimamizi wa vilabu na marais kwa maamuzi yao lakini mara chache huwa walengwa wa mashambulizi makali.
Ankaragucu iko katika nafasi ya 11 kwenye msimamo ikiwa na pointi 18, nafasi tatu chini ya Rizespor ikiwa na pointi 22 baada ya mechi 15.
Raundi inayofuata na ya 16 kati ya 38 ya ligi kuu ya Uturuki ilipangwa kufanyika wikendi ijayo.