Mkataba huo wa miaka 10 unatarajiwa" kwa kiasi kikubwa " kuimarisha juhudi za Serikali ya Somalia kulinda uhuru wake./ Picha: Ikulu Somalia

Meli ya jeshi la wanamaji la Uturuki imewasili katika Bandari ya Mogadishu kufuatia kusainiwa kwa makubaliano ya ulinzi na uchumi kati ya Somalia na Uturuki mwezi Februari mwaka huu.

Kinaliada F514 ilitia nanga bandarini Jumanne, miezi miwili baada ya mkataba wa kihistoria uliosainiwa kati ya nchi hizo mbili, ambapo Uturuki ilikubali kuipa Somalia msaada wa usalama wa baharini.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, mawaziri kadhaa, na balozi wa Uturuki nchini Somalia, Alper Aktas, walihudhuria sherehe ya kuwakaribisha.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, mawaziri kadhaa, na balozi wa Uturuki nchini Somalia, Alper Aktas, walihudhuria sherehe ya mapokezi. Picha: Ikulu Somalia

Akihutubia sherehe hiyo, Rais Mohamud aliisifu Uturuki kwa kusaidia Somalia mara nyingi, akiita "nchi ya kirafiki na ya kindugu", na akashukuru Ankara kwa makubaliano ya kulinda Somalia.

Aidha, ameishukuru Ankara kwa makubaliano ya ulinzi na kuongeza kuwa jeshi la wanamaji la Somalia sasa litakuwa na nguvu zaidi.

Waziri wa Ulinzi wa somalia Abdulkadir Mohamed Nur aliliambia shirika la Anadolu kwamba makubaliano hayo yanaashiria uhusiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

Mkataba wa 'kihistoria'

Mawaziri wa ulinzi wa Uturuki na Somalia walitia saini mkataba wa ushirikiano mwezi Februari ili kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na utulivu wa eneo hilo.

Mkataba huo ni mkataba wa miaka 10 ambao "kwa kiasi kikubwa" utaimarisha juhudi za Serikali ya Somalia kulinda uhuru wake, Waziri wa Habari Daud Aweis alisema baada ya mkataba huo kupata idhini ya bunge nchini mwake.

Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre vile vile aliusifu mkataba huo kama "wa kihistoria", akiishukuru serikali ya Uturuki na watu wake kwa msaada wao thabiti kwa serikali na watu wa Taifa la Pembe ya Afrika.

Ankara ina ubalozi wake Mkubwa barani Afrika mjini Mogadishu na pia ilijenga chuo chake kikubwa cha kijeshi nje ya nchi hiyo ili kufundisha jeshi la kitaifa la Somalia.

TRT World