Makala ya 'Holy Redemption' yaoneshwa katika tamasha la Al Jazeera la nchi za Balkani

Makala ya 'Holy Redemption' yaoneshwa katika tamasha la Al Jazeera la nchi za Balkani

Makala hiyo inaangazi udhalimu wa Waisraeli dhidi ya Wapalestina katika eneo linalokaliwa la West Bank.
Makala ya TRT ya Holy Redemption ilioneshwa kwenye tamasha la 7 la kimataifa la Al Jazeera la nchi za Balkani huko Sarajevo./Picha: Wengine  

Filamu ya TRT World ya 'Holy Redemption' ilioneshwa kwenye tamasha la 7 la kimataifa la Al Jazeera la nchi za Balkani huko Sarajevo, Bosnia na Herzegovina.

Makala hiyo iliyotengezwa kwenye mazingira magumu, inaangazia kwa undani mgogoro wa Israeli na Palestina.

Ikiwa imeongozwa na kutengenezwa na Jose Carlos Soares, Tanju Sahin, na Aslihan Eker Cakmak, filamu ya Holy Redemption ilirekodiwa miezi miwili baada ya kuanza kwa uvamizi huo katika eneo la Gaza, Oktoba 7.

Timu hiyo ilipitia upenyezaji mgumu katika vikundi vya walowezi wa Israel wenye itikadi kali katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu ili kukamilisha filamu hiyo. Akizungumza na mwandishi wa Anadolu, mkurugenzi wa filamu hiyo Soares alibainisha kuwa filamu hiyo inalenga kuwasilisha ukweli badala ya maoni. "Filamu haiakisi mawazo yetu. Katika dakika 53, hautapata tafakari yoyote ya kibinafsi. Utakachosikia ni mawazo ya kweli ya watu tuliowahoji,” alisema.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TRT  Omer Faruk Tanriverdi pia alihudhuria tukio hilo na Mkurugenzi wa Al Jazeera kwa nchi Balkani./Picha: Wengine

Mtayarishaji Aslihan Eker Cakmak alisisitiza mtazamo wa kipekee wa filamu hiyo, akilenga walowezi ambao wamezikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. "Kwa mara ya kwanza, hadithi hii inasimuliwa sio kwa macho ya Wapalestina ambao ardhi yao ilitwaliwa lakini kupitia kwa wavamizi, walowezi. Hao ndio wanaozungumza katika filamu hii,” Cakmak alisisitiza.

Pia aliangazia kujumuishwa kwa wanaharakati wa Israeli katika filamu, akitoa mtazamo mpana wa kazi inayoendelea. "Filamu hii inaonyesha jinsi Palestina inavyokaliwa, siku baada ya siku. Mtandao muhimu na maandalizi ya kina yalihitajika kuzalisha hili. Kama TRT World, tumefuatilia mradi huu kwa muda mrefu, na iliwezekana tu kupitia kuanzisha mawasiliano sahihi na kupata imani ya watu mashinani,” aliongeza.

TRT Afrika