Uturuki yataka uchunguzi wa kina ufanyike juu ya mauaji ya mwanaharakati wa Kituruki

Uturuki yataka uchunguzi wa kina ufanyike juu ya mauaji ya mwanaharakati wa Kituruki

"Aysenur alikuwa ni jasiri aliyehatarisha maisha yake kuanika uovu na ubabe wa Israeli, " amesema Mkurugenzi wa Mawasiliano.
"Aysenur ameuwawa na majeshi ya Israeli katika eneo la West Bank," alisema Altun katika mtandao wake kijamii.  

Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Ikulu ya Uturuki Fahrettin Altun ameitaka Marekani kuchunguza mauaji yaliyofanywa na Israeli dhidi ya mwanaharakati Aysenur Ezgi Eygi, ambaye pia ana uraia pacha wa Marekani na Uturuki.

"Israeli ilimlenga ili kuwanyamazisha wale wote wanaopaza sauti zao dhidi ya manyanyaso wanayofanyiwa Wapalestina." alisema Altun katika ukurasa wake wa X.

Akisisitiza kuwa tayari Uturuki ilikuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya Aysenur, Altun alisema, "Tunataka uchunguzi wa kimataifa. Kwa kuwa Aysenur alikuwa raia wa Uturuki na Marekani, Marekani lazima ifanye hivyo na kuishinikiza mamlaka ya Israeli kuwajibika."

"Ni lazima kwa jumuiya ya kimataifa kuacha tabia ya kupuuzia mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israeli. Mauaji ya kishahidi ya Aysenur ni mfano tosha wa namna Isareli inavyoendelea kutokujali. Ni wakati muafaka kwa Israeli kuanza kuwajibika. "

"Nafsi nzuri kama za Aysenur ambazo haziwezi kustahimili uonevu zitaingia katika historia kama mashujaa wa kweli waliopigania haki. Tunaheshimu sadaka yao na kumbukumbu zao kutoka chini ya mioyo yetu."

Eygi aliuwawa wiki iliyopita na majeshi ya Israeli katika eneo la West Bank wakati akishiriki maandamano ya amani dhidi makazi haramu ya Wayahudi katika eneo la Beita, Nablus.

Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Najah huko Nablus kilithibitisha kwamba aliuawa kwa risasi kichwani. Siku ya Ijumaa, mwili wake ulirejeshwa Uturuki kwa uchunguzi zaidi na mazishi . Matokeo ya awali kutokana na uchunguzi huo uliofanywa katika Taasisi ya Tiba ya Uchunguzi wa Izmir, ulifichua jeraha la kichwa lililosababishwa na jeraha la risasi kwenye sikio la chini.

Sababu ya kifo ilirekodiwa kama "kuvunjika kwa fuvu, kuvuja damu kwa ubongo, na uharibifu wa tishu za ubongo." Ilithibitishwa kuwa kulikuwa na jeraha la risasi kichwani mwake, lakini hakuna jeraha la kutokea. Vipande vya chuma vilivyopatikana kwenye kichwa vilichukuliwa kwa uchambuzi. Mashuhuda wanasema kuwa Eygi alikuwa kwenye shamba la mizeituni, mbali na eneo kuu la maandamano, alipouawa kwa kupigwa risasi.

Kulingana na kikundi cha ISM, kinachoongozwa na Wapalestina cha kupambana na uvamizi, Eygi "alilengwa kwa makusudi kabisa" na mshambuliaji huyo wa Kiisraeli.

Jonathan Pollack, shahidi wa mauaji hayo na mwanaharakati wa Israeli ambaye ameshiriki katika maandamano dhidi ya makazi haramu, alisema mwanajeshi aliyempiga risasi Eygi "alikuwa karibu kabisa na Eygi."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ilisema mauaji ya Eygi ni "matokeo ya moja kwa moja ya utekelezaji wa maagizo" ya wanasiasa wa Israeli ya kuwaua Wapalestina na wanaharakati wa mshikamano. Wizara hiyo iliitaka serikali ya Israeli kuwajibika kikamilifu kwa uhalifu huo ambao ulithibitisha mipango yake iliyotanguliwa ya kuzidisha hali hiyo ili kugharamia miradi yake ya kikoloni katika maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

TRT Afrika