Na
Ozan Ahmet Cetin
Wakati Kamati Tendaji ya Sekta ya Ulinzi ya Uturuki, inayosimamia sekta hiyo, ilipotangaza mradi wa kijeshi, Mfumo wa Ulinzi wa 'Steel Dome', wiki iliyopita, uliashiria hatua muhimu kwa uwezo wa ulinzi wa nchi.
Katika taarifa rasmi, Kurugenzi ya Mawasiliano ilielezea Mfumo wa Ulinzi wa 'Steel Dome' kama mpango wa kuunda mfumo kamili wa ulinzi wa anga.
Haluk Gorgun, Katibu wa Viwanda vya Ulinzi wa Uturuki, alifafanua kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kuwa vihisi vyote na mifumo ya silaha zinafanya kazi pamoja katika mtandao uliojumuishwa, na kuunda mfumo wa ulinzi wa anga wa umoja na uwezo wa kufanya kazi kwa wakati halisi. Pia alisema mfumo huo utatumia akili bandia kuwasaidia watoa maamuzi.
Mradi huo utawezesha uendeshaji mmoja wa mifumo mbali mbali ya ulinzi wa anga iliyotengenezwa na tasnia inayokua ya ulinzi nchini, ikijumuisha KORKUT, HİSAR A+, GÖKBERK, HİSAR-O, na SİPER.
Kando ya mifumo ya silaha, mfumo wa Steel Dome litaunganisha teknolojia ya rada na teknolojia ya 'electro-optical' (inayojumuisha uhandisi wa kiolektroniki), kuwezesha ufuatiliaji, utambuzi na uainishaji wa malengo chini ya mfumo uliyounganishwa.
Steel Dome ni mfumo wa kisasa unaoashiria hatua muhimu katika safari ya tasnia ya ulinzi ya ndani ya Uturuki.
Mfumo huu sio mwisho wa safari lakini ni mfumo unaoendelea kuboreka. Itaboreshwa daima, ikijumuisha teknolojia na uwezo mpya kadri zinavyoibuka.
Uturuki tayari imetengeza sehemu kubwa ya mfumo wa Steel Dome. Hata hivyo, kama maafisa wanavyosisitiza, ni mfumo wa mifumo ambayo inahitaji juhudi kubwa ili kutimia kikamilifu.
Kunaweza kuwa na vizuizi vinavyofanana na vile vinavyoathiriwa na miradi tata ya ulinzi kama vile kutengeneza ndege ya kivita ya F-35.
Kwa kujifunza kutokana na mifano hii, Uturuki inapaswa kukumbuka changamoto zinazoweza kutokea kama vile ucheleweshaji, ongezeko la gharama na hata kufeli.
Kushughulikia masuala haya mapema kunaweza kusaidia kuhakikisha mafanikio ya mradi huo.
Uturuki na safari ya ulinzi wa anga
Ulinzi wa anga kwa muda mrefu umekuwa wasiwasi mkubwa kwa Uturuki, haswa tangu Vita vya Ghuba mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati tishio la mashambulio ya makombora ya Scud lilipoibuka.
Kwa kujibu, Marekani, Ujerumani, na Uholanzi zilipeleka mifumo ya makombora ya Patriot hadi Uturuki chini ya uangalizi wa NATO. Zoezi hili liliendelea, huku NATO ikitoa mifumo ya ulinzi wa makombora kwa Uturuki kama inahitajika.
Baada ya muda, Uturuki ilikuja kuona utimilifu wa mahitaji yake ya ulinzi wa anga kama mtihani wa washirika wake kufahamu hofu wa nchi hio katika masuala ya usalama.
Katika miongo miwili iliyopita, Uturuki ilikabiliana na wasiwasi mkubwa wa kijiografia na kisiasa unaotokana na kukosekana kwa utulivu wa kikanda, migogoro inayoongezeka, na mwonekano unaoongezeka wa vitisho kutoka kwa watendaji wa kitaifa na wasio wa kitaifa.
Chini ya hali hizi, Uturuki iliamua inahitaji mifumo yake ya ulinzi wa anga ili kupambana majibu na changamoto zake za kipekee za usalama.
Hii ingeruhusu nchi kulinda anga yake kwa uhuru, bila kutegemea maamuzi ya kisiasa ya washirika wa NATO, ambayo wakati fulani ilipuuza wasiwasi wa usalama wa Uturuki.
Mnamo 2006, Ankara ilizindua mpango wa T-LORAMIDS (mfumo wa Ulinzi wa Ndege wa Muda Mrefu wa Kituruki na Mfumo wa Ulinzi wa Kombora), ikilenga kupata mfumo wa ulinzi wa masafa marefu wa anga na makombora.
Kufikia 2010, vipimo vya kiufundi vilikamilishwa, na wito wa mapendekezo ya kununua mifumo ya ulinzi ulitolewa.
Mpango huo ulivutia makampuni kadhaa ya kimataifa: makampuni ya Kimarekani Raytheon na Lockheed Martin walipendekeza mfumo wa Patriot, Eurosam ya ushirikiano wa Ufaransa na Italia ilitoa SAMP-T, Rosoboronexport ya Urusi iliweka mbele S-300, na CPMIEC ya China ilipendekeza FD-2000.
Mnamo 2013, baada ya Marekani kukataa uhamishaji wa teknolojia kwa mifumo ya makombora ya Patriot, Uturuki ilipitisha uamuzi wa muda mnamo Septemba 2013 wa kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa Uchina wa FD-2000.
Hata hivyo, kufikia Novemba 2015, Uturuki iliachana na ununuzi wa FD-2000 kutoka China kwa ajili ya uzalishaji wa ndani.
Majadiliano yaliyofuata kuhusu ununuzi wa mifumo ya Patriot kutoka Marekani pia hayakufaulu.
Katika kipindi hiki, Uturuki iliwekeza pakubwa katika kuendeleza mifumo yake ya ndani ya ulinzi wa anga kwa miinuko na masafa mbalimbali, kama vile KORKUT, HISAR-A, HISAR-O na SIPER.
Rais Erdogan alisema, "Tutafikia hatua ambapo tutaweza kuuza mifumo ya ulinzi wa anga kwa wale ambao, kwa kutumia visingizio mbalimbali, walikataa kutuuzia." Mfumo wa Steel Dome unawakilisha kilele cha juhudi hizi.
Mfumo wa ulinzi wa anga uliojumuishwa
Steel Dome ni mfumo jumuishi wa ulinzi wa anga (IADS), mtandao unaojumuihsa vihisi, silaha na mifumo mbalimbali ya mawasiliano ili kutambua, kufuatilia na kupunguza vitisho kwa ufanisi.
Kuhama kuelekea mfumo wa IADS kutoka kwa vijenzi tofauti vya ulinzi wa anga ni hatua ya kimantiki na muhimu, kwani inaboresha ufanisi wa utendaji wa uwezo uliopo wa ulinzi wa anga ili kushughulikia changamoto za vita vya kisasa.
IADS huhakikisha kuwa mifumo ya ulinzi wa anga binafsi inafanya kazi kwa umoja, ikitumia uwezo wa kila mfumo huku ikifidia udhaifu wake. Ujumuishaji huu huboresha nyakati za kujibu hujuma na kupunguza mapengo ya ufikiaji.
Ujumuishaji wa vitambuzi mbalimbali na mitandao ya mawasiliano ndani ya IADS hutoa picha ya kina na ya wakati halisi ya anga. Ujumuishaji huu ni muhimu kwa kutambua na kuweka kipaumbele kwa vitisho vya kisasa vya anga, ikiwa ni pamoja na ndege za siri na makombora ya kuhujumu angani.
Zaidi ya hayo, IADS inaruhusu ugawaji bora wa rasilimali za ulinzi.
Udhibiti huhakikisha kwamba mfumo wa silaha unaofaa zaidi unatumiwa dhidi ya kila tishio, kuzuia utumiaji wa kupindukia au utumiaje wa vifaa viliyikuwa vichache.
Kwa mfano, mifumo ya hali ya juu ya SAM inaweza kushughulikia malengo makubwa, ilhali mifumo ya bei ya chini na inayopatikana kwa urahisi zaidi vinaweza kushughulikia vitisho vya hali ya chini.
HAKİM, mfumo wa kwanza wenye na udhibiti wa anga nchini, utakuwa uti wa mgongo wa mfumo wa Steel Dome kutekeleza kazi hii. Iliyoundwa kikamilifu na wahandisi wa Kituruki, HAKİM imeundwa kusaidia na kuunganisha mifumo ya vihisi na silaha, na kuunda mtandao wa ulinzi wa anga wa kina na unaoingiliana.
Hii inajumuisha teknolojia za kizazi kipya kama vile Mfumo wa RadNet, Rada ya EİRS, na mifumo ya makombora ya ulinzi wa anga ya HİSAR na SİPER.
Sawa na mfumo wa udhibiti wa anga wa NATO, inaweza kudhibiti rada za tahadhari za mapema na kuunganisha data ya rada kutafuta, kutambua na kufuatilia ndege.
Faida ya ziada ya IADS ni kwamba katika hali ya mzozo, inahakikisha kwamba kushindwa au uharibifu wa kitenzi kimoja haulemazi mtandao.
Umuhimu mkubwa wa IADS ni ikiwa betri moja ya rada au kombora itatolewa, zingine zinaweza kujaza pengo.
Ustahimilivu huu ni muhimu katika kuhimili mashambulizi ya kusambaa na kuhakikisha ulinzi unaoendelea.
Vitisho vya anga vinaendelea kubadilika, huku wapinzani wakiendeleza teknolojia ya hali ya juu kama vile makombora ya hypersonic na uwezo wa vita vya kielektroniki.
IADS inaweza kusasishwa na kuboreshwa kwa urahisi zaidi kuliko mifumo inayojitegemea, ikiruhusu ujumuishaji wa teknolojia na mbinu mpya.
Kubadilika huku kunahakikisha kuwa uwezo wa ulinzi unabaki kuwa muhimu na mzuri dhidi ya vitisho vinavyoibuka.
Changamoto za mfumo wa mifumo
Ingawa mfumo wa Steel Dome, kama IADS, linatoa faida nyingi, pia linajumuisha ugumu na hatari zinazoambatana na mifumo ya ulinzi ya hali ya juu.
Kama ilivyo kwa mfumo wowote wa mifumo, ujumuishaji wa vijenzi vingi huleta changamoto ambazo lazima zidhibitiwe kwa uangalifu ili kuhakikisha mafanikio ya kiutendaji.
IADS huunganisha vijenzi vingi tofauti—rada, makombora ya kutoka ardhini hadi angani, ndege za kukatiza hujuma, na vituo vya kuamrisha na kudhibiti—ili kuwa mfumo kamili nzima.
Muunganisho huu unahitaji programu ya hali ya juu ya data programu ya komputa na 'hardware', majaribio makali, na uratibu wa kina.
Utata unaweza kusababisha masuala katika ushirikiano, huku kila mfumo mdogo ukihitaji kuwasiliana na kufanya kazi na mifumo mengine.
Hili lilikuwa changamoto muhimu katika mradi wa F-35, shughuli ngumu sawa ya ulinzi, ambapo kuunganisha vifaa vya ndege vya hali ya juu, teknolojia ya siri, na uwezo wa majukumu mengi ulihitaji utatuzi wa kina na uboreshaji wa mara kwa mara.
Utata wa kuunganisha aina mbalimbali za mifumo midogo mara nyingi husababisha ucheleweshaji.
Kila sehemu lazima ijaribiwe kwa kina, kwa kujitegemea na ndani ya mfumo jumuishi, ili kuhakikisha kuaminika na utendaji.
Ucheleweshaji katika sehemu moja ya mfumo unaweza kupungua, na kuathiri ratiba nzima ya mradi. Hata hivyo, baadhi ya vipengele vya Dome ya Chuma tayari vinafanya kazi.
Ugumu wa mfumo wa mifumo mara nyingi husababisha gharama kubwa kuliko inavyotarajiwa. Haja ya teknolojia ya hali ya juu, majaribio ya kina, na maendeleo ya mara kwa mara huongeza gharama.
Mpango wa F-35, kwa mfano, ni karibu dola bilioni 180 zaidi ya makadirio ya awali ya gharama. IADS, inayotegemea vitambuzi vya hali ya juu, mitandao ya mawasiliano, na mifumo ya kisasa ya kuamrisha na kudhibiti, vile vile huathiriwa na gharama zinazoongezeka.
Kando na hilo, kudumisha IADS juu ya uendeshaji pia kunaweza kuwa changamoto na gharama kubwa. Ujumuishaji wa mfumo unamaanisha kuwa uboreshaji wowote au ukarabati wa sehemu moja unaweza kuhitaji marekebisho kwa mifumo mengine.
Changamoto ya ziada ni kuathiriwa na mashambulizi ya mtandao. Kuunganisha vigenzi vingi katika mfumo mmoja huongeza eneo la mashambulizi ya mtandao yanayoweza kutokea.
Kuhakikisha usalama wa mtandao wa IADS kunahitaji umakini na masasisho ya mara kwa mara, kwani udhaifu katika mfumo mmoja mdogo unaweza kuathiri mtandao mzima.
Mradi wa F-35 umekabiliwa na wasiwasi sawa wa usalama wa mtandao, kutokana na utegemezi wake kwenye mifumo ya mtandao na ushiriki mkubwa wa data.
Mradi wa Steel Dome ni uthibitisho wa uwezo wa Uturuki unaokua wa kutengeneza masuluhisho ya hali ya juu ya ulinzi yanayolenga changamoto zake za kipekee za usalama.
Walakini, mafanikio ya mradi hayategemei tu uvumbuzi wa kiteknolojia lakini pia juu ya upangaji wa kimkakati na maono ya mbele.
Kutarajia na kushughulikia vikwazo vinavyowezekana, kama vile ucheleweshaji wa maendeleo, kuongezeka kwa gharama, na udhaifu wa usalama wa mtandao, itakuwa muhimu ili kuhakikisha ufanisi na uthabiti wa mfumo kwa muda mrefu.
Mwandishi, Ozan Ahmet Cetin, ni mhadhiri msaidizi wa Internet Governance Lab na mshirika wa utafiti wa Center for Security, Innovation and New Technology in Washington D.C. Yeye pia anasomea PhD katika Shule ya School of International Service at American University, ambapo anasoma teknolojia zenye athari za usalama wa taifa.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.