Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani vikali kuchomwa kwa nakala ya Quran, kitabu kitakatifu cha Waislamu, nchini Sweden juma liliyopita, huku akiongeza kuwa mashambulizi dhidi ya maadili matakatifu "hayawezi kutajwa kama uhuru wa mawazo".
"Mashambulizi hayo yote ya kashfa dhidi ya misikiti na kitabu kitakatifu hayawezi kukubalika," Erdogan alisema baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri katika mji mkuu Ankara siku ya Jumatatu.
Kabla ya hayo, awali, Waziri wa Mambo ya nchi za Kigeni wa Uswidi Tobias Billstrom alisema matukio kama hayo yangeweza kubadili "taswira nzuri" ya nchi hiyo na kuwa mbaya "iwapo itaendelea kuonyeshwa kama yenye chuki dhidi ya Uislamu."
Akizungumza na jarida la kila siku ya Sydsvenskan mapema Jumatatu, Billstrom aliongeza kuwa ni "vigumu kutabiri mambo yatakayofuata katika mchakato wa kuidhinishwa kwa uanachama wa NATO wa Uswidi," ikizingatiwa kutoridhishwa kwa Uturuki kuridhia Uswidi kujiunga na NATO.
Siku ya Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswidi ilishtumu vikali kuchomwa kwa nakala ya Qur'an nje ya Msikiti Mkuu wa Stockholm mnamo Juni 28, ikiwa ndio siku ya kwanza ya sikukuu ya sherehe za Waislamu ya Eid al Adha.
"Uhuru wa kujieleza hulindwa vikali nchini Uswidi. Lakini maana yake sio kuwa Serikali inaunga mkono maoni yoyote inayotolewa. Mikusanyiko ya hadhara ambayo inaruhusiwa pia inaweza kugeuka kuwa yenye ubaguzi na ya kukera." wizara ilifafanua.
"Maandamano kama hayo yaliyofanyika Jumatano ni hivyo tu. Na pia yana madhara makubwa kwa usalama wa ndani na usalama wa Uswidi Iliongeza,"
Erdogan ameongoza kuwa Uturuki inatumai matukio ya hivi majuzi yaliyotokea kufuatia mauaji yaliyotekelezwa na polisi wiki iliyopita nchini Ufaransa, yatafikia kikomo "haraka iwezekanavyo," na kukatiza mzunguko wa ghasia unaoongezeka.
Uturuki ina wasiwasi kuwa huenda matukio hayo yatachochea "wimbi jipya la shinikizo na vitisho" dhidi ya wahamiaji na Waislamu, aliongeza.
"Matukio yaliyoanza Ufaransa na muda mfupi baadaye kuenea hadi nchi nyingine yana asili yake katika usanifu wa kijamii iliyozalisha mawazo haya," Erdogan alisisitiza.
"Katika nchi zinazofahamika kwa ukoloni wao wa zamani, ubaguzi wa rangi wa kitamaduni umegeuka kuwa ubaguzi wa kitaasisi."
Maandamano yameitikisa Ufaransa tangu Jumanne wiki iliyopita, baada ya afisa wa polisi kumpiga risasi Nahel Merzouk, mwenye umri wa miaka 17 na asili ya Algeria, wakati wa ukaguzi wa trafiki katika kitongoji cha Nanterre jijini Paris huku akidaiwa kupuuza amri ya kusimama.
Polisi wa Ufaransa walitia mbaroni watu 157 kwenye operesheni ya usiku kucha kufuatia maandamano ya nchi nzima dhidi ya mauaji ya polisi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti Jumatatu.
Afisa aliyempiga risasi Nahel anakabiliwa na uchunguzi rasmi kwa mauaji ya hiari na amewekwa katika kizuizi cha mapema.