Klabu ya Uturuki ya Fenerbahce imemsajili mchezaji nyota maarufu na nahodha wa Bosnia na Herzegovina Edin Dzeko kutoka klabu ya Inter Milan ya Italia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37, amerejea mjini Istanbul akiwa mwana Fenerbahce baada ya kushiriki fainali ya Ligi ya mabingwa akiichezea Inter ambapo walipoteza dhidi ya Manchester City mapema mwezi huu.
Dzeko, aliyeisaidia Manchester City, kuinua taji lao la kwanza la Ligi kuu ya England ndani ya miaka 44, alikamilisha usajili wake baada ya kupitia uchunguzi wa afya katika Hospitali mjini Istanbul na kutia wino mkataba wa miaka miwili kuanzia msimu wa 2023-24 na 2024-25.
Akizungumza na Fenerbahce TV baada ya kutia saini mkataba wake, Edin Dzeko ameusifu uamuzi wake kwa kuwa wenye hekima.
"Nimejawa na mchanganyiko wa hisia. Ingawa tayari nilikuwa najua ukubwa wa klabu ya Fenerbahce, muda mfupi tu baada ya kutua hapa, nimegundua kuwa nilifanya uamuzi bora na siwezi kusubiri kuingia uwanjani." Alisema Dzeko.
''Nawahakikishia mashabiki wetu, nitajitahidi katika kila mechi tutakayocheza na katika kila mazoezi tutakayofanya.'' aliongeza.
Fenerbahce, ilitwaa ubingwa wa Kombe la Ziraat na kumaliza katika nafasi ya pili katika ligi kuu ya Uturuki nyuma ya Galatasaray.
Dzeko anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora zaidi wa timu ya taifa ya Bosnia, na aliisaidia timu hiyo kushiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza mnamo 2014.