Wachezaji wa Galatasaray wakisherehekea ubingwa wao./Picha: AA

Klabu ya Galatasaray imetwaa taji la 24 la Ligi Kuu ya Uturuki baada ya kuifunga Tumosan Konyaspor 3-1.

Galatasaray ilianza kuhesabu mabao dakika ya 29 ya mchezo kupitia kwa mchezaji wa kimataifa wa Argentina Mauro Icardi aliyepiga kichwa kilichomshinda mlinda lango Jakub Slowik wa Tumosan Konyaspor.

Icardi aliongeza goli la pili katika dakika ya 51 baada ya kufunga kwa kisigino kufuatia kazi nzuri ya Lucas Torreira, kabla ya kiungo wa Galatasaray Berkan Kutlu hajahitimisha karamu ya magoli, dakika chache baadaye.

Louka Prip aliifungia Konyaspor bao la kufutia machozi katika dakika ya 78, matokeo ambayo yaliipa Galatasaray ubingwa wa 24 wa Turkish Super Lig.

Galatasaray imetwaa taji hilo baada ya kufikisha alama102.

Wachezaji na viongozi wa Galatasaray waliingia uwanjani mara baada ya filimbo ya mwisho kusherehekea ubingwa wao.

Tumosan Konyaspor inashika nafasi ya 16 ikiwa na alama 41 na hivyo kusalia kwenye Ligi Kuu ya Uturuki katika msimu ujao.

MKE Ankaragucu ilikubali kichapo cha mabao 4-2 katika uwanja wa Trabzonspor na kushuka daraja. Klabu hiyo kutoka mji mkuu wa Uturuki ilikuwa na alama 40 kumaliza msimu wa 2023-24 katika nafasi ya 17.

TRT Afrika