Sasa ni wazi kuwa uhusiano kati ya Samatta na Fenerbahce umefika kileleni baada ya kocha mpya wake Ismail Kartal kueleza kuwa Samatta hayupo kwenye mipango yake msimu huu.
Kocha Kartal amenukuliwa akisema hayo, alipokuwa akifafanua sababu za kutokuwepo kwa Samatta kwenye kikosi cha wachezaji wa Fenerbahce watakaoshiriki Kombe la ‘Pari Premier Cup’ utakaoanza hapo kesho St. Petersburg, Urusi, hadi tarehe 15 Julai.
Nyota huyo wa zamani wa Klabu ya Simba, na TP Mazembe, alijiunga na Fenerbahce kutoka Aston Villa ya Uingereza msimu wa 2020-2021 na kutia sahihi mkataba wa hadi 2024. Lakini sasa, amewekwa kwenye orodha ya wachezaji watakouzwa kwenye dirisha la uhamisho kabla ya msimu ujao.
Kulingana na orodha rasmi ya wachezaji 33 wa Fenerbahce watakaosafiri, Mbwana Samatta ameachwa nje licha ya kuwa kati ya kikosi cha Fenerbahce kwa kumaliza mkataba wake wa mkopo na klabu ya Ubelgiji ya RC Genk.
Siku za Samatta Fenerbahce zilionekana kuwa za kuhesabika pindi iliponoa safu yake ya ufungaji kwa kumsaini Edin Dzeko kutoka Inter Milan, na hatua hiyo ikipunguza nafasi za Samatta kikosini.