Samatta amesaka changamoto mpya Ugiriki huku nyota yake ikizidi kung’aa tangua alipjitangaza kwenye ulingo wa soka / Picha: AA

Mfungaji hodari wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta amesaini mkataba wa miaka miwili na PAOK ya Ugiriki.

'Samagoal' alikatiza mkataba wake na miamba wa Uturuki, Fenerbahce, ambapo aliichezea mechi 30 na kufunga magoli 6 kufuatia uhamisho wake kutoka Aston Villa.

Staa huyo aliimiminia Fenerbahce sifa na kuitakia kila la heri kwenye ujumbe kupitia ukurasa wake wa Instagram.

“Kwa wapenzi Fenerbahce, nasema asante sana kwa kunipa fursa ya kucheza katika mojawapo ya vilabu kubwa barani Uropa. Katika kipindi nilichokuwepo, nimejifunza mengi sana, na Ingawa naondoka, kwa hakika mtakuwepo moyoni mwangu milele. Ninawatakia kila la kheri na natumai mtabeba vikombe vingi sana siku za usoni. Yasafener”

Uhamisho wa Samatta kuelekea Ugiriki unajiri baada ya nyota huyo kuitumikia Genk ya Ubejgiji kwa njia ya mkopo kutoka Fenerbahce msimu uliopita. Mnamo msimu wa 2021- 22 Fenerbahce ilimuachilia kwa njia ya mkopo hadi Royal Antwerp kabla ya kurejea Uturuki kuendelea na huduma kwenye timu hiyo

Samatta amesaka changamoto mpya Ugiriki huku nyota yake ikizidi kung’aa tangua alipjitangaza kwenye ulingo wa soka

Akiwa TP Mazembe, Samatta aliisaidia timu hiyo kutwaa mataji manne ya ligi huku akiwa mfungaji bora wa ligi ya DRC na mfungaji bora pia katika ligi ya vilabu bingwa Afrika, 2015.

Mnamo 2016, Samagoal, alitunukiwa mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya Afrika na kuwa mwanasoka wa kwanza Kutoka Afrika Mashariki kupokea tuzo hiyo.

Fomu yake kwenye TP Mazembe ilimzolea ofa ya kuelekea Ubelgiji na hakuchelea kujizolea sifa kemkem alipotua RC Genk. Aliibuka mfungaji bora wa ligi ya Ubelgiji mnamo msimu wa 2018-19 na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi ya Ubelgiji ya Jupiler Pro League. Aliifungia timu hiyo mabao 76, ndani ya mechi 191 alizocheza

Samatta sasa anatarajiwa kushiriki michuano ya raundi ya pili kufuzu kwa ligi ya bara Ulaya ya UEFA Europa Conference msimu ujao itakapochuana na klabu ya Beitar Jerusalem.

Kufuatia ufanisi wake kwenye soka ya kulipwa katika vilabu mbalimbali, kilichosalia sasa kwa Samatta ni kuvunja rekodi ya mfungaji mwenye magoli mengi zaidi timu ya taifa ya Tanzania inayoshikiliwa na nyota mstaafu Mrisho Ngassa.

TRT Afrika