Na Emmanuel Onyango na Tuğrul Oğuzhan Yılmaz
Hatimaye, jitihada za Uturuki zimezaa matunda, baada ya Somalia na Ethiopia kumaliza tofauti zao.
Uturuki imefanikiwa kuzipatanisha nchi hizo zilizokuwa kwenye mgogoro wa karibu mwaka mmoja, ukichochewa na mpango wa Addis Ababa na eneo lililojitenga la Somalind kuhusu bandari la Bahari Nyekundu, jambo lililoiudhi Mogadishu.
Siku ya Jumatano, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara kwa kikao kilichochukua saa saba.
Wote wawili, Abiy na Sheikh Mohamud walikubaliana kuheshimiana na kuheshimu utawala wa kila upande, na kuihakikishia Ethiopia ufikiaji wa bahari hiyo.
Maelewano hayo yamefifisha wasiwasi wa mgogoro mkubwa katika eneo la Pembe ya Afrika, huku Umoja wa Afrika na umoja wa nchi za IGAD zikipongeza hatua ya Uturuki.
Katika taarifa yake, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alimpongeza Rais Tayyip Erdogan kwa kuunga mkono pande hizo mbili katika azma yao ya kumaliza tofauti zao.
Umoja wa Mataifa, uliielezea hatua hiyo kama hatua muhimu kufikia urafiki wa kweli. "Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa jitihada za Uturuki kwa kuzileta pande hizi mbili pamoja, viongozi wa nchi hizi mbili kwa maelewano,"alisema msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric.
Workneh Gebeyehu, ambaye ni Katibu Mtendaji wa IGAD alimshukuru Rais Recep Tayyip Erdogan kwa nafasi yake katika maridhiano hayo.
Kilichokubaliwa
Uhasama kati ya nchi hizo jirani zilianza mwezi Januari 2024 baada ya Ethiopia kuazima eneo la kilomita 20 la pwani ya eneo linalotaka kujitenga la Somaliland, huku Ethiopia ikiiahidi Somaliland kuwa itaitambua kama eneo huru.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alianzisha mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo kupitia mchakato wa Ankara wa Julai 2024, ikiendesha mazungumzo na ujumbe kutoka nchi hizo mbili.
Mazungumzo hayo yaliangazia masuala nyeti kwa nchi zote mbili huku jitihada za Uturuki zikizaa matunda.
"Ni ishara ya mafanikio makubwa katika sera ya mambo ya nje ya Uturuki. Baada ya miezi sita ya jitihada hizo, tumefikia maamuzi yenye maana sio tu kwa Uturuki, Somalia na Ethiopia, bali kwa usalama wa Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu," alisema Dkt Tunç Demirtaş, mtaalamu wa mahusiano kati ya Uturuki na Afrika kutoka Chuo Kikuu cha Mersin.
Kupunguzwa kwa uhasama
Uhasama kati ya Somalia na Ethiopia uliibua hofu kuu katika eneo zima la kanda huku jitihada za mataifa ya Afrika Mashariki kama vile Kenya na Uganda zikigonga ukuta.
Kulingana na mchakato wa Ankara, ujumbe kutoka Somalia na Ethiopia utaanza majadiliano yanayoratibiwa na Uturuki kabla ya mwisho wa mwezi wa Februari mwaka 2025, na kutakiwa kumaliza majadiliano hayo ndani ya miezi minne.
Nchi hizo mbili, pia zimeonesha utayari wao wa kumaliza tofauti zingine zozote zitakazojitokeza, kupitia msaada wa Uturuki.
"Makubaliano hayo yanazuia migongano zaidi. Uturuki, taifa lenye nguvu ya kidiplomasia na uhusiano na Somalia na Ethiopia ina nafasi ya kipekee sana katika maridhiano hayo," amesema Demirtaş.
Nafasi ya Uturuki
Uamuzi wa Uturuki kuwa msuluhishi wa mazungumzo wa mgogoro kati ya Somalia na Ethiopia, unadhihirisha uhusiano wa muda mrefu kati Uturuki na nchi hizo mbili. Pia inaonesha kuaminiwa kwa mchakato wa Ankara.
Rais Erdogan alionesha imani yake na makubaliano hayo, akilitakia eneo la Pembe ya Afrika amani, utulivu na ustawi, akisema ni mfano wa maeneo mengine yenye uhusama ulimwenguni.
"Bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Hata hivyo, huu ni mkataba muhimu kwa ajili ya mustakabali wa baadae. Hali hii inadhihirisha ushawishi wa Uturuki katika Pembe ya Afrika," alisema Demirtaş.
"Taswira ya Uturuki kama mshirika wa kutumainiwa inaongeza imani kwa nafasi ya nchi hiyo kwenye utatuzi wa migogoro mingine," aliongeza.
"Lazima tuzungumzie uhusiano wa kihistoria kati ya Somalia na Uturuki ambao unakwenda mbali zaidi ya Jamhuri ya sasa ya Uturuki hadi kwenye enzi za utawala wa Ottoman," alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ali Omar, kabla ya mazungumzo ya Ankara.
‘’Tangu mwaka 2011, Rais Erdogan, wakati huo akiwa Waziri Mkuu wa Uturuki alipoitembelea Somalia, uhusiano kati ya nchi hizi mbili umekuwa kwa kasi sana,’’ Omar alisema.
"Uturuki imeisaidia Somalia katika nyanja nyingi ikiwemo usalama, maendeleo pamoja na sekta ya mafuta,’’ aliongeza.
"Uturuki ina nafasi ya kipekee katika ukanda huo, hususani uhusiano wake kati na Somalia pamoja na Ethiopia ambao unaanzia kipindi cha Ottoman," alisema Dkt Fatma Yildiz, mtaalamu wa masuala ya Afrika kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town.
"Ethiopia ina idadi ya watu na uchumi unaokuwa kwa kasi huku ikikabiliwa na changamoto ya kuwa nchi isiyo na eneo la bahari, ikiitegemea zaidi Djibouti kwa ajili ya masuala ya biashara. Hivyo basi, suala la kupata njia ya kuifikia bahari ni jambo la muhimu sana kwa Ethiopia. Kwa upande mwingine, Somalia bado inaonesha wasiwasi kuhusu utawala wake hususani kutokana na uwepo wa Ethiopia,” aliongeza.
“Azimio hili ni la muhimu sana kwa watu wa Ethiopia na Somali, kwa uhusiano kati ya Uturuki, Ethiopia, na Somalia na katika kutatua migogoro katika Pembe ya Afrika na bara zima kwa ujumla."