Shirikisho la Soka la Uhispania litafanya mkutano wa dharura siku ya Jumatatu huku rais wake, Luis Rubiales, akikabiliwa na kusimamishwa kazi na FIFA na dhoruba ya ukosoaji kutokana na madai kwamba alimpa mchezaji busu isiyohitajika kwenye midomo baada ya Uhispania kushinda Kombe la Dunia la Wanawake.
Rubiales amekataa kujiuzulu kutokana na tukio hilo na mchezaji Jenni Hermoso Jumapili iliyopita mjini Sydney, akisema busu hilo lilikuwa la makubaliano.
Wachezaji na msururu wa makocha kwenye kikosi cha wanawake wanadai aondoke, na serikali pia inataka aondoke.
Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) limeita mashirikisho ya kanda kwenye mkutano "wa kipekee na wa dharura" "kutathmini hali ambayo shirikisho hilo linajikuta" kufuatia kusimamishwa kwa Rubiales, msemaji wa RFEF alisema Jumapili.
Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA lilifungua kesi za kinidhamu dhidi ya Rubiales siku ya Alhamisi na kutangaza Jumamosi kuwa amesimamishwa kwa miezi mitatu kutoka kwa shughuli za soka za kitaifa na kimataifa kusubiri uchunguzi.
Kuthibitisha 'kutokuwa na hatia'
Rubiales, 46, alisema atatumia uchunguzi wa FIFA kuonyesha kutokuwa na hatia.
Rubiales alicheza hasa katika divisheni ya pili ya ligi ya Uhispania katika taaluma iliyochukua miaka 12. Alipochaguliwa kuongoza RFEF mnamo 2018, aliahidi kusasisha muundo wake, kuongeza mauzo na kufanya shirikisho hilo kuwa wazi zaidi.
Serikali ya Uhispania haiwezi kumfukuza kazi Rubiales lakini imekashifu vikali hatua yake na kusema Ijumaa ilikuwa inataka kumsimamisha kwa kutumia utaratibu wa kisheria mbele ya mahakama ya michezo.
Ghasia hizo zimekuja katika nchi ambayo masuala ya jinsia yamekuwa mada kuu katika miaka ya hivi karibuni.