Juhudi za klabu ya JKT Queens ya Tanzania za kuwa na msimu wenye mafaniko hazijaambulia patupu baada ya Shirikisho la Soka Afrika kutambua mchango wa klabu hiyo, wachezaji wake na kocha wake kwa soka ya wanawake barani Afrika msimu huu, 2023.
Vilevile, baada ya kuiletea Tanzania sifa kwa kutwaa kombe la CECAFA kwa vilabu bingwa vya wanawake Afrika Mashariki na kuiwakilisha Afrika Mashariki katika Ligi ya Mabingwa ya wanawake CAF, JKT Queens imeteuliwa kugombea Tuzo mbalimbali ikiwemo klabu bora ya mwaka upande wa wanawake Afrika.
Licha ya kuwa katika kundi gumu pamoja na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa ya wanawake CAF Mamelodi Sundowns na SC Casablanca ya Morocco iliyofika fainali, JKT Queens haikutoka mikono mitupu kwani ilifanikiwa kuifunga Athletico Abidjan 2-1 mechi ya makundi, Ligi ya mabingwa ya wanawake CAF, Cote d'Ivoire.
JKT Queens imeteuliwa kugombea tuzo ya klabu bora ya mwaka upande wa wanawake Afrika.
Aidha, nyota wake, Winifreda Gerald, ameteuliwa kugombea tuzo ya Chipukizi bora wa mwaka kwa upande wa wanasoka wa kike barani Afrika.
Winifreda Gerald ametambulika kwa kuifungia JKT bao la kusawazisha dhidi ya Athletico Abidjan mechi ya Ligi ya mabingwa ya wanawake CAF, na ambaye pia alikuwa mfungaji bora katika mashindano ya shule za CAF yaliyofanyika Afrika Kusini.
Mlinda lango wa timu hiyo, Najiat Abass Idrisa ameteuliwa miongoni mwa walinda langu 10 bora Afrika kwa upande wa wanawake ambapo atawania tuzo ya kipa bora wa mwaka kwa upande wa wanawake.
Wakati huo huo, Kocha wa JKT Queens, Esther Charuma ameweka historia kwa kuwa tu mmoja wa wakufunzi wawili wa kile walioteuliwa kugombea tuzo ya mkufunzi bora wa mwaka kwa upande wa wanawake.
Kocha Esther Charuma wa JKT Queens na Kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini Desiree Ellis ndio wanawake wawili tu kati ya makocha 10 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo na CAF.
Mnamo mwezi Agosti, Jkt Queens ilifuzu ligi ya mabingwa ya wanawake CAF baada Ya kuilaza klabu ya Benki ya Biashara ya Ethiopia kwa mabao 5-4 kwenye penalti katika mechi ya kufuzu kwa timu za cecafa.