''Hongerz kwa kina dada wetu, wamechora historia, mbele ya macho yetu tukishuhudia...''
Pongezi isiyo kifani kutoka kwa waziri wa michezo wa Kenya Ababu Namwamba.
Hii inafuatia kichapo cha 2-0 {5-0} kwa jumla dhidi ya Burundi na kufuzu kwa mara ya kwanza kwa Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake chini ya miaka 17 mkondo wa pili wa mchujo wa raundi ya nne uliofanyika Jumapili Uwanja wa Ulinzi Complex, Nairobi.
''Hongera kwao, na vile vile kwa Wakenya, kwa namna wamechangamkia na kufika kuwashabikia, Kwa mara ya kwanza uwanja huu wa ulinzi umeshona kushona...'' alielezea waziri Namwamba.
Timu hiyo imefuzu kwa kombe la dunia la FIFA kwa wanawake wasiozidi miaka 17 litakalochezwa kuanzia Oktoba 16-Novemba 3 mwaka huu nchini Dominican Republic.
Timu 16 zitashiriki mchuano huo.
Lorna Faith, mshambuliaji wa Kenya ndiye aliyechangamsha mechi dakika ya kwanza tu aliposhtua kwa goli la haraka dhidi ya kipa wa Burundi Clairia Nshirimana japo bao hilo lilikataliwa kwa kuvizia. Kunako dakika ya nane Marion Serenge lijaribu bahati yake lakini Mshambuliaji Nekesa alimharibia kwa kuvizia.
Hata hivyo ilitosha kuwapa Wakenya hao chipukizi uelewa wa mianya ya Burundi na wakatumia fursa hiyo kurindima shuti baada ya shuti.
Kipa wa Kenya Velma Auma, alijikuta hana shughuli kabisa baada ya kikosi cha ulinzi kinachoongozwa na nahodha wa timu Elizabeth Ochaka na wenzake Christine Adhiambo, Kimberly Akinyi na Lorine Ilavonga.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Starlets Mildred Cheche alipongeza kikosi chake akisema sasa wanalenga kujiandaa kikamilifu kwa kazi kubwa inayowakabili.
''Kwa sasa tunapumzika, lakini tunataka kujiimarisha kimkakati. Tunataka kwenda huko kama washindani wakali na sio tu kama washiriki wa kujaza namba,'' alisema Cheche. ''Ushindi huu una umuhimu sana sio kwetu pekee bali kwa taifa zima,'' aliendelea kusema.
Kenya inaungana na Nigeria na Zambia kama timu tatu za Afrika zitakazocheza Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 17 nchini Jamhuri ya Dominika mwezi Oktoba.
Nigeria ilikuwa timu ya kwanza ya Kiafrika kupata nafasi katika mashindano ya vijana ya wanawake baada ya kuishinda Liberia kwa jumla ya mabao 6-1.
Baada ya ushindi wao wa 3-1 katika mchezo wa kwanza Zambia waliwabana Morocco sare tasa usiku wa kuamkia leo na kujikatia tiketi.
Junior Starlets ni timu ya pili ya Afrika Mashariki kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 17, kufuatia majirani zao Tanzania, waliofika fainali za 2022 nchini India.