Meneja Thomas Tuchel anasaka taji la Bundesliga / Picha: AFP

Bayern Munich ya Ujerumani imetangaza kuwa wataachana na meneja Thomas Tuchel mwishoni mwa msimu, huku mabingwa hao wakijitahidi kusalia kwenye mbio za taji la Bundesliga.

"Tulifikia uamuzi wa pande zote kumaliza ushirikiano wetu katika msimu wa joto," Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Jan-Christian Dreesen alisema katika taarifa, kufuatia mazungumzo na Tuchel.

Dreesen ameongeza kuwa Bayern itafuta "mwelekeo mpya" chini ya kocha mpya msimu ujao.

Kuondolewa kwa Tuchel kunajiri baada ya kushindwa mara tatu mfululizo, ikiwemo kupoteza 3-0 dhidi ya wapinzani wa ligi Bayer Leverkusen.

Zikiwa zimesalia mechi 12 kabla ya msimu kumalizika, Bayern imejipata na pointi nane nyuma ya Bayer Leverkusen inayoongozwa na Xabi Alonso, ambao hawajapoteza hata mechi moja msimu huu.

Tangu ilipofungwa na Leverkusen, Bayern ilishuhudia fomu mbaya ikiwemo kupoteza 1-0 dhidi ya Lazio ya Italia katika raundi ya 16, Ligi ya Mabingwa na kupoteza 3-2 dhidi ya bochum kwenye ligi.

Bayern ilimteua Tuchel kuwa kocha wake baada ya kufukuzwa Chelsea mwishoni mwa 2022.

AFP