Wapenzi wa soka nchini Burundi wakiongozwa na Shirikisho la soka nchini humo, wanazidi kummezea mate, Irankunda, nyota mwenye umri wa miaka 17 aliyesajaliwa na klabu ya FC Bayern ya Ujerumani.
Irankunda alizaliwa mnamo 2006, Kigoma katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania, baada ya wazazi wake Gideon na Dafroza Irankunda, kutafuta hifadhi nchini Tanzania kufuatia vita vya ndani nchini Burundi.
Mnamo mwezi Agosti, rais wa shirikisho la soka la Burundi FFB, Alexandre Muyenge alifika Australia na kukutana na Irankunda na familia yake.
Irankunda mwenyewe amedumisha upendo wake kwa Burundi kwani amekuwa akiweka bendera ya Burundi kwenye kurasa zake zote za mitandao ya kijamii mara kwa mara.
Baadaye, nyota huyo mwenye umri wa Miaka 17 na familia yake, walihamia Australia, ambapo alianza safari yake ya soka.
Irankunda alisainiwa kutoka klabu ya ligi kuu ya Australia A-League, Adelaide United kwa kitita kinachoripotiwa kufika hadi pauni milioni £3m, ikiwa ni pamoja na ada zaidi.
Senti hizo zimevunja rekodi ya uhamisho wa ligi ya Australia iliyowekwa na uhamisho wa Marco Tilio alipojiunga na klabu ya Celtic FC kwa £1.5m gharama kubwa zaidi wakati huo.
Irankunda alitiwa saini na Adelaide United, maarufu Reds akiwa na umri wa miaka 15, 2021.
Aidha, nyota huyo atajiunga na wachezaji wenzake wa Bayern baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu ya wanaume wa 2023/24 unaoendelea.
"Ninafurahi kuwa na haya yote yamekamilishwa. Kujiunga na mojawapo ya vilabu bora ulimwenguni ni ndoto ya kweli kutimia. Nimefanya kazi kwa bidii kujaribu na kuifanya familia yangu ijivunie."Nestory Irankunda alisema.
Mshambuliaji huyo, anayeiwakilisha timu ya taifa ya Australia, atajiunga na Bayern kucheza rasmi ifikapo tarehe 1 Julai 2024 kwa mujibu wa mkataba wa muda mrefu aliosaini na mabingwa hao wa Ujerumani.
Hii ni kwa sababu Irankunda atakuwa ana miaka 18 tarehe 9 Februari 2024.
Kwa sasa, Irankunda ni mchezaji wa kikosi cha Australia na ameichezea upande wa timu hiyo kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 lakini tayari ameitwa kwa timu ya wakubwa.
Irankunda ameifungia timu ya taifa ya Australia kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 mabao 11 ndani ya mechi saba tu huku bado akisubiri nafasi yake ya timu ya wakubwa.
Tayari, winga huyo amecheza mechi 39 na klabu ya Adelaide United, huku akifunga mabao tisa na kutoa pasi mbili za magoli, huku akitarajiwa kuongeza idadi hiyo kufikia mwisho wa msimu huu unaoendelea.
Mnamo Machi 2023, Irankunda alikaribia kuweka historia na kuwa mchezaji mdogo zaidi kuiwakilisha Australia katika historia baada ya kuitwa kwenye kikosi kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ecuador. Hata hivyo hakuingia uwanjani kwani alisalia kwenye benchi.
Wengi wanaomba Irankunda akubali ombi la kuichezea Burundi na ili aweze kuchangia pakubwa safari ya timu hiyo kufuzu kombe la dunia 2026 ikiwa tayari imeanza safari hiyo kwa kushinda mechi moja, na kupoteza moja.
Iwapo ataichagua Burundi badala ya Australia, Irankunda atafuata nyayo za mchezaji mwingine aliyeichagua Burundi, Saido Berahino.
Licha ya kuiwakilisha England katika vikosi vya wachezaji wa chini ya miaka 16, U21, kwa jumla ya mechi 48 na hata kufunga mabao 25 kati ya 2008 na 2015, Saido Berahino alichagua Burundi.
Ndoto yake ilitimia mnamo 2018, wakati shirikisho la soka duniani FIFA, lilipomruhusu kuliwakilisha Burundi kwenye mechi za kimataifa.
Chini ya sheria za kubadili uwakilishi za FIFA, Irankunda anaweza kuichezea Burundi kwa kubadilisha mataifa ikiwa kwani wazazi wake ni kutoka Burundi. Aidha, bado hajaiwakilisha timu ya taifa ya Australia zaidi ya mara tatu au kwa zaidi ya miaka mitatu yaani hata hajaonekana katika mashindano makubwa kwa timu hiyo.