Wachezaji wa timu hiyo waligoma kushikana mikono na wapinzani wao wa Israeli, na kuutoa ushindi wao mkubwa kwa watu wa Palestina. / Picha: AA

Timu ya taifa ya mpira wa miguu kwa Walemavu ya Uturuki imelaani mashambulizi ya Israeli dhidi ya Gaza kufuatia ushindi wao mabao 6-0 dhidi ya Israeli katika michuano ya Ulaya iliyofanyika nchini Ufaransa.

Baada ya kuongoza kwa mabao 2-0 katika kipindi cha kwanza katika mtanange huo wa kundi C, Uturuki iliondoka na karamu ya magoli 6-0, baada ya filimbi ya mwisho katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Camille Fournier, ulioko mashariki ya Ufaransa, siku ya Jumapili.

Timu hiyo, maarufu kama 'Nyota na Mwezi', waligoma kupeana mikono na wapinzani wao kutoka Israeli, huku wakitoa ushindi huo mkubwa kwa ajili ya watu wa Palestina.

Baada ya mchezo huo, wachezaji hao walifanya dua maalumu na kuonesha mshikamano kwa Waislamu wa eneo la Gaza.

Takriban miezi minane ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yamewaua zaidi ya Wapalestina 36,000 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto - na kukata usambazaji wa chakula, maji na dawa, na kuifanya sehemu kubwa ya eneo lililozingirwa kuwa kwenye baa la njaa.

Uturuki, ambayo ni mabingwa watetezi wa Ulaya, watakutana na Azerbaijan katika mchezo wao wa kundi hilo utakaofanyika siku ya Jumatatu.

Timu mbili bora kutoka kila kundi zinatagemewa kufuzu kwa hatua ya robo fainali, katika michuani hiyo yenye kushirikisha timu 16.

TRT Afrika