Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesisitiza kuwa Ame alikuwa ni miongoni mwa wachezaji 23 waliokuwa wameorodheshwa kwa ajili ya mechi dhidi ya Guinea.
Kulingana na TFF, kabla ya mechi hiyo ya iliyochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Novemba 19, wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) walikaguliwa na timu pinzani pamoja na kamishna wa mchezo huo, kabla ya kuruhusiwa kucheza.
“TFF haina taarifa yoyote kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuwa ushiriki wa Ame katika mechi hiyo haukuwa halali,” ilisomeka taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa X wa TFF.
Mapema Novemba 21, Shirikisho la Soka la nchini Guinea (Feguifoot) limetuma malalamiko yake kwa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), likipinga ushindi wa Tanzania dhidi ya Guinea.
Katika taarifa yake ya Novemba 20, Feguifoot inaituhumu Tanzania kwa kumuingiza uwanjani Muhamed Ibrahim Ame akiwa amevaa jezi namba 26 badala ya 24 kama ilivyokuwa imeorodheshwa na CAF.
Feguifoot pia imetilia shaka uwezo wa kamisaa wa mchezo huo, Francis Oliele kutoka Kenya, ikimtuhumu kwa kuipendelea ‘Taifa Stars’ kwakuwa wanatokea kanda moja ya CECAFA.
Kulingana na kanuni namba 47 ya fainali za mataifa ya Afrika, kosa hilo linaweza kusababisha kuondolewa kwa timu hiyo kwenye mashindano hayo na kusimamishwa kwa chama cha soka cha nchi hiyo.
Taifa Stars iliifunga timu ya taifa ya Guinea bao 1-0, na hivyo kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za AFCON 2025, zitakazofanyika nchini Morocco mwakani.