Washington Wizards wamezindua akaunti za mitandao ya kijamii kwa lugha ya Kiarabu kama njia moja ya kukuza brandi yao Mashariki ya Kati. Chaneli @WizardsArabic tayari iko hewani kwenye mtandao wa Twitter na Instagram pamoja na heshitegi maalum kwa ajili yao #yallaWizards
Akaunti hizo za mitandao ya kijamii zitatumika kwa ajili ya kutoa habari kwa wafuatiliaji kuhusu matokeo na uchambuzi wa mechi na maudhui mengine yanayohusu timu hiyo ya basketiboli. Aidha pia kuna mpango wa kuzindua tovuti maalum kwa lugha ya Kiarabu, lengo kubwa likiwa ni kukuza Brandi ya Washington Wizards.
“Tuna furaha kuongeza lugha ya Kiarabu kwenye akaunti zetu za mitandao ya Kijamii,” anasema Afisa wa Biashara wa klabu hiyo Jim Van Stone.
“Tunajua mashabiki wetu kutoka Uarabuni sasa watafuatilia kwa karibu zaidi,” anaongeza Jim.
Aidha inatarajiwa pia hatua hiyo itawaleta karibu mashabiki kutoka Uarabuni waishio Columbia, Maryland na Virginia nchini Marekani.
Wizards wamejitahidi pakubwa kuukuza mchezo wa basketiboli kupitia kliniki na program nyengine za kuupa mchezo huo sifa katika jamii. Aidha pia wapo kwenye mkatanba wa ushirikiano na Shirika la ndege la Etihad kwa lengo hilo hilo la kukuza mchezo huo.
Wizards pia wana akaunti kwa lugha ya Kihispania @vamoswizards ambayo ilizinduliwa mwezi uliopita.
Ikumbukwe mwaka uliopita Wizara ya Utamaduni na Utalii ya Abu Dhabi ilitangaza kusaini mkataba na NBA na baadae kukashuhudiwa mechi za basketiboli katika Uwanja wa Etihad huko Abu Dhabi, ikiwemo mechi ya Milwaukee Bucks dhidi ya Atlanta Hawks.