Hossam Hassan (K), Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri, Rais wa shirikisho la Soka la Misri Gamal Allam na Ibrahem Hasan, mkurugenzi wa soka wa timu ya taifa. / Picha: AFP

Mfungaji bora kwa miaka yote nchini Misri, Hossam Hassan ndiye kocha mpya wa Timu ya taifa ya nchi hiyo, maarufu ‘Mafarao’, Chama cha Soka cha Misri (EFA) kimetangaza.

Hassan anachukua mikoba ya Mreno Rui Vitoria, baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika michuano ya AFCON iliyomalizika hivi karibuni.

EFA, inayoongozwa na Gamal Allam, ilimpa Vitoria mkono wa kwaheri Februari 4, baada ya Mafarao hao kutolewa na DRC kwa mikwaju ya penati, katika hatua ya timu 16 bora.

Aidha, Misri, ambayo imebeba taji la AFCON kwa mara saba, hawakupata ushindi wa hata mechi moja kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ya 34 yaliyofanyika Cote D’ivoire.

Hassan, kocha wa zamani wa Zamalek, Masry, na Ismaily, pia anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote Misri akiwa ametia kimiani mabao 69 katika mechi 178.

Kibarua cha kwanza cha Hassan kuiongoza Mafarao kitakuwa nchini UAE mwezi Machi wakati Misri itashiriki katika mashindano ya kimataifa ya kirafiki na Croatia, New Zealand, Na Tunisia.

TRT Afrika