Rais wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales amejiuzulu kufuatia shutuma kali kwa kumpiga busu Jenni Hermoso mdomoni katika sherehe za ushindi wa Kombe la Dunia la Wanawake Agosti 20 mwaka huu.
Rubiales ambaye tayari amesimamishwa kazi alituma kujiuzulu kwake kwa rais wa mpito wa shirikisho hilo, na pia alielezea uamuzi wake wa hatimaye kujiuzulu katika mahojiano ya televisheni.
"Ndio nitajiuzulu kwa sababu siwezi kuendelea na kazi yangu," Rubiales, mwenye umri wa miaka 46 alisema wakati wa kipindi cha televisheni cha "Piers Morgan Uncensored".
Rubiales alizua tafrani duniani kote baada ya kumbusu kwa lazima kiungo Hermoso wakati wa sherehe ya medali kufuatia ushindi wa Uhispania wa Kombe la Dunia mjini Sydney mnamo Agosti 20.
Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) Jumapili usiku lilithibitisha katika taarifa yake kujiuzulu kwa Rubiales.
Baada ya awali kukataa kujiuzulu, FIFA ilimsimamisha kwa muda kwa siku 90, wakati waendesha mashtaka wa Uhispania wamefungua kesi dhidi yake kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia.
Hermoso, 33, alikuwa amewasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kitaifa siku ya Jumanne, akimshutumu rasmi Rubiales kwa unyanyasaji wa kijinsia.
Rubiales, ambaye anasisitiza kwamba busu hilo lilikuwa la ridhaa, alisema hataki soka la Uhispania lidhurike na "kampeni isiyo na uwiano" dhidi yake.
“Nina imani na ukweli na nitafanya kila niwezalo ili ushinde,” aliandika.
Rubiales alisema kuondoka kwake kutachangia "utulivu" katika ombi la Kombe la Dunia la wanaume la 2030 ambalo Uhispania itashiriki.
Baadhi ya wanasiasa wa Uhispania walipongeza kujiuzulu kwa Rubiales.