Nahodha wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars na staa wa klabu ya Qatar ya Al Duhail Michael Olunga ameeleza kuwa yeye na wenzake wana ari ya kuonyesha mchezo wenye nguvu na wa hali ya juu dhidi ya Al Nasr ya Saudi Arabia na kujiandikishia matokeo mazuri huku wakilenga ushindi wao wa kwanza wa kampeni yao ya, Kundi E Kombe la mabingwa Asia, maarufu AFC Champions league.
Al Nassr, inayosaka ushindi wake wa tatu mfuflulizo, ilianza ligi hii ya mabingwa bara Asia AFC msimu wa 2023/24 vyema kwa kuzishinda Persepolis FC ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran 2-0 na FC Istiklol ya Tajikistan 3-1.
Olunga ameongeza kuwa ingawa wanaiheshimu Al Nasr kwa kuwa na wachezaji wenye majina makubwa kama vile Ronaldo na Mane, hilo sio tatizo kwao
"Al Nasr iko na wachezaji kadhaa maarufu ambao wamefanikiwa kushinda mataji mengi katika soka yao kama vile Christano Ronaldo, Sadio Mane na Talisca, hata hivyo hatukabiliani na kila mchezaji kivyake bali tuna cheza dhidi ya timu kamili. Bado tunapaswa kuzingatia lengo letu kuu kuja na matokeo mazuri ambayo yatatusaidia kuendelea na safari yetu ya Asia," Olunga alieleza.
Olunga ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumanne katika ukumbi wa mikutano wa waandishi ulioko kwenye uwanja wa First Park, nchini Saudia.
"Maandalizi yetu ya mechi hii yamekuwa mazuri, kila mtu yuko tayari kwa mchuano huo, na kila mmoja wetu anaheshimu uwezo wa wachezaji wa Al Nasr. Tunajua kwamba tunapaswa kujifanyia kazi ili kufanya mechi kali kama timu," Olunga alisema.
Al Duhail inaelekea katika mchuano huo ikishikilia nafasi ya 3 kwenye jedwali ikiwa na alama moja huku nayo Al Nasr yuko juu ya kikundi na alama 6.
"Mchuano huu una umuhimu mkubwa kwetu, na lazima tuondoke na matokeo mazuri, na ili kufikia lengo hili, lazima tumheshimu mpinzani wetu na kufanya juhudi zetu zote uwanjani. Lazima tuwe wa kweli kwamba tuko katika nafasi ya tatu katika kikundi, lakini haiwezekani kurudi na kufuzu kwa raundi inayofuata," alimaliza.
Al Duhail, walitinga nusu fainali ya ligi hii ya mabingwa bara Asia kwa mara ya kwanza msimu uliopita ambapo waliondolewa, na wanaingia kwenye mechi hii wakiwa chini ya kocha mpya, Mfaransa Christophe Galtier aliyechukua nafasi ya Muargentina Hernan Crespo.
Aidha, ushindi utazidisha matumaini ya timu ya Saudi Arabia ya AL Nassr inayoongozwa na mastaa akiwemo Cristiano Ronaldo kutua hadi kwenye hatua ya raundi ya timu 16 bora.
Al Nassr inaingia mchuano huu ikisherehekea kumbukumbu ya miaka 68 hii leo tangu uanzilishi wake mnamo 1955.