Baada ya kuisaidia Tanzania kutua Afcon Côte d'Ivoire mwaka ujao, kiungo wa kushoto wa Taifa Stars, Novatus Miroshi, anatarajiwa kuwa Mtanzania wa tatu tangu Mbwana Samatta na Kassim Manara kushiriki mechi ya UEFA Champions League.
Macho ya mashabiki wa soka Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla yatakuwa uwanjani Volksparkstadion, Hamburg, Ujerumani usiku huu wakati kiungo chipukizi Novatus Miroshi na klabu yake ya Shakhtar itakapokuwa inakwaruzana na FC Porto ya Ureno.
Miroshi ambaye alijiunga na Shakhtar Donetsk kwa njia ya mkopo kutoka klabu inayoshiriki ligi kuu ya Ubelgiji ya Zulte Waregem, amejumuishwa katika kikosi kilichosafiri kuelekea Ujerumani ambapo Shakhtar itacheza mechi zake za Ligi ya Mabingwa nje ya Ukraine kwa sababu za vita kwa msimu wa pili mfululizo.
Mnamo Septemba 2019, Mtanzania mwingine Mbwana Samatta aliweka historia kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa wakati Klabu yake ya zamani Genk ya Ubelgiji ilipopigwa 6-2 na klabu ya Salzburg.
"Kwa Samatta nitafika, ninaamini nitafika. Hiyo ndio ndoto yangu," Ilikuwa ndio kauli ya Novatus Miroshi katika mahojiano yake na mojawapo ya televisheni nchini Tanzania mnamo 2020.
Miroshi alikuwa mvuto mkubwa alipokuwa akipiga ligi ya Tanzania akiziwakilisha Azam FC na Biashara United mbali na kujumuishwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania mara kwa mara.
Kiungo huyo alitawazwa chipukizi bora wa mwaka kwenye ligi kuu ya Tanzania msimu wa 2019.
Kutoka Future Stars, kuelekea Azam hadi Biashara United Agosti 2019 kwa njia ya mkopo, kisha kufululiza hadi Beitar Tel Aviv Bat Yam ya Israel kwa msimu mzima wa 2021/22, kisha Maccabi Tel Aviv FC na hatimaye S.V Zulte Waregem ya Ubelgiji, kwa kweli safari ya Novatus hadi Shakhtar imekuwa ni ndefu lakini huenda urefu wa safari yake ukaja na ufanisi mwingi iwapo atatinga uwanjani dhidi ya FC Proto.