Kuwasili kwa Victorien Adebayor huko Amazulu kumecheleweshwa bila kuepukika licha ya mpango huo kukamilika. Picha RS Berkane

Adebayor amekwama Niamey na kushindwa kusafiri hadi Afrika Kusini au kupata visa yake kutokana na hali ya mapinduzi ya Julai 26 licha ya kusaini Amazulu ya Afrika Kusini baada ya kulengwa na vilabu mbalimbali vikiwemo Simba ya Tanzania.

Hali ya mapinduzi nchini Niger, imemzuia mfungaji wa nchi hiyo Zakaria Victorien Adebayor kusafiri huku mshambuliaji huyo akikosa njia ya kuondoka nchini humo kuelekea Afrika Kusini na hata kukosa kupewa visa ya kusafiri.

Victorien Adebayor alikuwa miongoni mwa wachezaji 9 wapya ambao walitangazwa hivi majuzi na Rais wa AmaZulu, Sandile Zungu huku wakitazamia kuongoza safari yao ya kutwaa taji katika kampeni ya msimu wa 2023/24.

Licha ya klabu ya Amazulu FC ya ligi ya Afrika kusini maarufu 'Usuthu' kumtambulisha mfungaji huyo hivi majuzi baada ya kumwahi kutoka mabingwa wa Kombe la mashirikisho ya CAF, Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco, bado hajajiunga na wenzake.

Aidha, kutofika kwa straika hiyo imeathiri matokeo ya timu hiyo inayoshiriki ya Ligi Kuu ya DStv ya Afrika Kusini na kuilazimu kuanza mechi zake mbili za kwanza msimu huu wa 2023-2024 bila kufunga bao.

Kocha wa Klabu ya Amazulu, Pablo Franco Martin Zakaria amelalamikia kuhusu hilo baada ya kuanza ligi kwa sare mbili bila mabao.

"Tulimsajili mshambuliaji lakini anasubiri visa yake kutolewa," alisema Martin.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, alikuwa mfungaji bora katika misimu iliyopita ya Kombe la Shirikisho la CAF akiwa na mabao 6 huku pia akiisaidia Berkane kushinda CAF Super Cup msimu uliopita.

Zakaria Adebayor ndiye mfungaji bora zaidi katika historia ya timu ya taifa ya Niger, baada ya kufikisha mabao 18 katika mechi 43 na kumpiku Moussa Maazou ambaye alikuwa akishikilia rekodi hiyo hapo awali.

TRT Afrika