#LFO05 : Athlétisme: marathon de Chicago / Photo: AFP

Ingawa macho yote na mazungumzo yamekuwa juu ya bingwa Kelvin Kiptum, anayeshikilia rekodi ya Dunia ya mbio za Marathon kwa wanaume, mipango inaendelea ya mazishi ya kocha wake, Gervais Hakizimana, ambaye pia alihusika katika ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vyao.

Mwili wa kocha huyo Gervais Hakizimana ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Eldoret, tangu kifo chake Jumapili, Februari 11, 2023.

Serikali ya Kenya kupitia wizara ya michezo, imesaidia kumsafirisha Kocha huyo , kukamilisha shughuli ya mazishi.

Hata hivyo, familia ya Hakizimana ilipuuza matokeo ya ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na kuonyesha kuwa mkufunzi wa mbio za marathon alifariki kutokana na jeraha la kichwa.

Wameiomba serikali ya Kenya ianzishe uchunguzi kubaini sababu hasa ya kifo cha mwanafamilia wao.

Gervais Hakizimana, Kocha wa Kiptum ni nani?

Hakizimana mwenyewe ni mwanariadha, aliyeishi Ufaransa miaka mingi, ambapo alishinda mbio mbalimbali, zikiwemo na 2008 Beaufort Half Marathon na 2011 Ferrette Half Marathon.

Gervais Hakizimana alihamia Kenya mnamo 2006, kutoka Rwanda akikaribia mwishoni mwa ujana wake, na kufanya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya riadha ya 2007 World Cross Country Championships.

Hakizimana na Kelvin Kiptum waliungana 2013, wakati Kiptum akiwa mwanariadha chipukizi.

Hakizimana alishindana London Marathon 2016, lakini hakumaliza kwa sababu ya jeraha. Eliud Kipchoge alitwaa ubingwa wakati huo kwa muda wa 2:03:05,

Aidha, aligeuka kuwa mkufunzi mwenye mafanikio baada ya kutofanikiwa katika mbio za masafa marefu.

Kabla ya kukutana na kifo chao, Kiptum na kocha wake Hakizimana walikuwa wakilenga mbio za Rotterdam Marathon za mwezi Aprili, ambapo Kiptum alinuia kuwa mkimbiaji wa kwanza rasmi wa mbio za marathon kushinda kwa chini ya saa mbili katika historia.

Kiptum pia angekutana ana kwa ana na Eliud Kipchoge kwenye mashindano ya Olimpiki Paris, mshindi wa mbio mbili za Mwisho za Olimpiki za wanaume.

TRT Afrika na mashirika ya habari