Mkenya Rhonex Kipruto asherehekea ushindi wa shaba katika Mashindano ya Riadha ya Dunia ya 2019 mjini Doha. Picha / Reuters  

Rhonex Kipruto amepigwa marufuku kwa miaka sita kwa matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, Kitengo cha Uadilifu wa Riadha (AIU) kilisema Jumatano, huku Mkenya huyo akitarajiwa kupoteza rekodi yake ya dunia ya mbio za barabarani za kilomita 10 na medali ya shaba ya ubingwa wa dunia.

Kipruto, mwenye umri wa miaka 24, ambaye alishinda medali ya shaba kwenye mbio za mita 10,000 katika mashindano ya dunia mwaka 2019, alikuwa amesimamishwa kwa muda kwa ukiukaji wa sheria za kupambana na dawa za kuongeza nguvu Mei mwaka jana. Sasa amepigwa marufuku hadi Mei 2029.

Kipruto alivunja rekodi ya dunia ya mbio za barabarani za kilomita 10 mwaka 2020 huko Valencia na alishinda mbio za mita 10,000 kwenye Ligi ya Almasi ya Stockholm mwaka 2019 - matokeo ambayo sasa yatabatilishwa.

Mahakama ya kinidhamu iliamua kwamba kulikuwa na hitilafu katika Pasipoti ya Kibiolojia ya Mwanariadha (ABP) ya Kipruto, ambayo inaonyesha tofauti ambazo zinaweza kufichua athari za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu.

Sahihisho: Katika taarifa iliyochapishwa Juni 5, 2024, picha ya Conseslus Kipruto ilitumika kimakosa kutokana na majina ya pili kufanana. Kwa sababu Conseslus Kipruto hana uhusiano na mada husika, picha iliyohusishwa imesahihishwa.

Makala hii imehaririwa upya Oktoba 14, 2024 baada ya kutokea kwa mchanganyiko wa picha katika makala ya awali.

Reuters